Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini imeitaka Wizara ya Nishati kuendelea kuusimamia ipasavyo Mradi wa Kuzalisha Umeme kwa Julius Nyerere (JNHPP) ili ukamilike kwa wakati. 

Hayo yameelezwa na Makamu Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Mhe. Kirumbe Ng'enda leo Septemba 07, 2024 wakati wa ziara ya kukagua hatua za utekelezaji wa mradi huo ambao utaingiza megawati 2,115 mara baada ya kukamilika.

"Wizara iendelee kusimamia kwa umakini mradi huu ili mashine zote Tisa ziweze kukamilika kama ilivyopangwa." Amesema Mhe. Ng'enda

Aidha, kamati hiyo imeipongeza Serikali kwa kuhakikisha mashine zilizosalia zinaendelea kukamilika na kufanya kazi ambapo hadi sasa zimekamilika mashine tatu ambazo zinazalisha kiasi cha megawati 705 na mashine namba sita ipo kwenye hatua za mwisho  kukamilishwa.

Kwa upande wake Naibu Waziri Nishati, Mhe. Judith Kapinga amesema Wizara ya Nishati imekuwa ikifanya kazi kwa ushirikiano na kamati hiyo ya Bunge ikiwa ni pamoja na kupokea maelekezo, ushauri na mapendekezo ya Kamati.

"Kazi kubwa ya Kamati ni kutusimamia sisi Serikali, na sisi tunahakikisha kuwa maelekezo yenu yote yanatekelezwa na mafanikio yake yanaonekana katika miradi mbalimbali kama JNHPP ambao utekelezaji wa mradi wake umefikia asilimia 98." Amesema Kapinga

Ameongeza kuwa, Wizara  ya Nishati chini ya Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati,  Mhe. Dkt. Doto Biteko itaendelea kuusimamia mradi huo ila ukamilike kwa wakati.

Ameeleza kuwa, Mkandarasi wa mradi ameshalipwa takriba shilingi trilioni 6.3 kati ya shilingi trillioni 6.5 zinazopaswa kulipwa.



Na Mwandishi Wetu,Manyara .

Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya kuzalisha vinywaji changamshi ya Mati Super Brands Limited David Mulokozi amejitokeza kujiandikisha kwenye daftari la kudumu la Wapiga kura katika kituo Cha Bagara Sekondari Wilayani Babati Mkoani Manyara huku akieleza kufurahishwa na zoezi hilo linaloendeshwa kwa ufanisi mkubwa na Tume Huru ya Uchaguzi na kuwataka wakazi wa Mkoa huo kujitokeza kwa wingi.

Mulokozi amesema kuwa zoezi hilo linafanyika kwa utaratibu mzuri ambao unamuwezesha kila mwananchi kujiandikisha na kuendelea na shughuli za uzalishaji mali bila kuathiri ratiba zao za kila siku.

“Mimi leo nimetimiza haki yangu ya kujiandikisha ili niweze kushiriki Uchaguzi wa Serikali za mitaa na Uchaguzi Mkuu 2025 na imechukua dakika chache kwasababu nilishawahi jiandikisha hivyo nilikua nahamisha taarifa zangu kuja hapa ninapoishi sasa hivi” Anaeleza Mulokozi.

Mulokozi amewataka vijana na wakazi wa mkoa huo kwa ujumla kujitokeza kwa wingi kujindikisha kwani zoezi hilo halichukui muda na hakuna foleni.

Pia amesema kuwa amehamasisha wafanyakazi wa viwanda vyake kujiandikisha na wameweka utaratibu unaowapa fursa ya kujiandikisha.

kwa Upande wake Afisa mwandikishaji Msaidizi Jimbo la Jabati Mjini Bahati Baltazari kutoka Tume Huru ya Uchaguzi (INEC) Akizungumzia hali ya Uandikishaji amesema kuwa mwitikio wa wananchi umekua mkubwa na wa kuridhisha na kuwataka wananchi kuendelea kujitokeza.


 

Na: Josephine Majura, WF, Mwanza


Wakuu wa Idara ya Ununuzi na Wakuu wa Idara ya Mipango wameahidi kwenda kutekeleza kwa vitendo yote waliyojifunza kupitia mafunzo ya kuwajengea uwezo katika Sheria mpya ya Ununuzi, Sheria ya Ubia  kati ya  Sekta ya  Umma na Sekta Binafsi na Matumizi sahihi ya Takwimu yaliyohusisha mikoa ya Mwanza, Geita na Kagera yaliyofanyika katika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mwanza.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti baada ya kupatiwa mafunzo hayo Afisa Mipango na Uratibu kutoka Halmashauri ya Wilaya ya Kwimba, Bw. Rogatevane Kipigapasi,  aliishukuru Serikali kwa kuwajengea uwezo kuhusu Sheria hizo kwa kuwa mafunzo hayo yatawaongezea uwezo na weledi katika kutekeleza majukumu yao.

“Kulikuwa na mada nzuri binafsi nimejifunza fursa zilizopo kupitia Sheria ya Ubia kati ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi, marekebisho katika Sheria hii yanatoa fursa kwa wazawa kushiriki katika utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo”, alisema Bw. Kipigapasi.

Afisa Mipango wa Halmashauri ya Wilaya ya Chato, Bi. Maria Ndohelo, alishauri  mafunzo hayo yawe endelevu kwa kutolewa mara kwa mara ili kuhakikisha Sheria, Kanuni na Taratibu zinajulikana vizuri kwa watumiaji wakuu wa Sheria hizo ili iwe rahisi wakati wa utekelezaji.

“Nina waasa Washiriki wenzangu wa mafunzo haya kwenda  kuyatumia vizuri tutakaporudi katika Vituo vyetu  vya kazi kwa kuwa Serikali ina matarajio makubwa kwetu sisi baada ya mafunzo haya”, alisema Bi. Ndohelo.

Alifafanua kuwa Serikali inawategemea kama wataalamu waliopewa dhamana katika kupanga Mipango ya Serikali na kusimamia Manunuzi mbalimbali ya Umma hivyo ni jukumu la kila mshiriki wa mafunzo kwenda kufanya kazi kwa weledi kama walivyoelekezwa katika mafunzo.

Mafunzo hayo yamewashirikisha Wakuu wa Idara ya Ununuzi na Wakuu wa Idara ya Mipango wa mikoa ya Mwanza, Geita na Kagera yaliyofunguliwa na Kaimu Katibu Tawala wa Mkoa wa Mwanza Bw. Kusirie Swai katika ukumbi wa Ofisi  ya Mkuu wa Mkoa wa Mwanza.
Kaimu Katibu Tawala wa Mkoa wa Mwanza, Bw. Kusirie Swai, aliwataka Washiriki wa mafunzo kwenda kutekeleza majukumu yao kwa kuzingatia Sheria, Kanuni na Taratibu.

Bw. Swai alisema kuwa Serikali hutunga sheria ili kuhakikisha wanaotekeleza majukumu kwa niaba ya Serikali wanazifuata, ili kupata matokeo chanya yanayotarajiwa na Serikali.

Wizara ya Fedha kwa kushirikiana na Taasisi zake ikiwemo Mamlaka ya Udhibiti wa Ununuzi wa Umma (PPRA), Kituo cha Ubia kati ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi (PPPC) na Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) wanaendelea kutoa mafunzo ya kuwajengea uwezo Wakuu wa Idara ya Ununuzi na Mipango nchi nzima katika mikoa ya Kikanda ikiwemo Kanda ya Ziwa, Kanda ya Kati, Kanda ya Pwani, Kanda ya Kaskazini, Kanda ya Kusini, Kanda ya Nyanda za Juu Kusini na Kanda ya Magharibi.



 Na Chedaiwe Msuya,WF


Wizara  ya Fedha imehitimisha utoaji wa mafunzo kuhusu Sheria ya Ununuzi kwa Umma  katika mikoa ya Mtwara, Lindi na Ruvuma.

Mafunzo hayo yaliyofanyika katika Manispaa ya Mtwara Mikindani mkoani Mtwara ili yakilenga kuwapa uelewa kuhusu Sheria mpya ya Ununuzi wa Umma Sura namba 410. 

Kaimu Mkurugenzi wa Huduma za Kisheria kutoka Kituo cha Ubia kati ya Sekta ya Umma na Sekta binafsi (PPPC), Bi. Flora Tenga alisema kuwa malengo ya mafunzo yalikuwa kuwaelimisha maofisa mipango na viongozi wote wanaohusika na ununuzi ili kufahamu fursa zilizopo katika Sheria hiyo na namna wanavyokwenda kuitekeleza. 

"Sheria ya Ubia kati Dekta ya Umma na Sekta Binafsi imetoa fursa mbalimbali katika miradi ya ubia ambapo kuna fursa na vivutio vingi vinavowavutia wawekezaji huku lengo lingine ni kuhusu Sheria ya Ubia kati ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi, Sura Na. 103 iliyofanyiwa marekebisho mbalimbali na kutoa fusa mbalimbali katika miradi ya ubia," alisema Bi. Flora

Lifafanua kuwa kuna fursa nyingi, kuna vivutio vya kikodi na visivyo vya kikodi ambavyo vinavutia wawekezaji na kuna vivutio mbalimbali ambavyo wanataka kuwaelimisha wanaotekeleza miradi ya ubia.

Pia amewataka  wanaotekeleza miradi ya maendeleo, badala ya kusubiri  fedha za Serikali kutekeleza miradi hiyo  watumie Sheria hiyo kumwalika mbia mwekezaji aweze kuleta fedha za kutekeleza miradi hiyo ya maendeleo ikiwemo miradi midogo midogo inayotekelezwa kwenye Serikali za Mitaa

Vilevile alisema kuna Sheria ya Takwimu kwani maendeleo au mipango yoyote haiwezi kupatikana bila kujua takwimu zilizopo.

"Kwahiyo tuko hapa pia kuwaelimisha Maafisa Mipango na viongozi wengine namna ya kutumia Takwimu sahihi"alisema Bi. Flora

Naye Meneja wa Mamlaka ya Usimamizi wa Ununuzi wa Umma (PPRA) Kanda ya Kusini, Fenias Manasseh alisema kuwa wamelazimika kutoa mafunzo hayo kwa watumishi wa Serikali kutoka sekta mbalimbali ili kuwapatia elimu hiyo ya Sheria ya Ununuzi wa Umma ili  waweze kujua fursa na mabadiliko yaliyopo kwenye Sheria hiyo ili waweze kufaidika nazo.

"Wengi wao hapa wanataka katika Taasisi Nunuzi wanaofanya kazi ya michakato ya ununuzi sasa kama hawaelewi mabadiliko yaliyojitokeza kwenye Sheria ya Ununuzi wa Umma wataendelea kuwa na mambo ya kizamani na kusababisha wahusika washindwe kufaidi hizi fursa nyingi mbalimbali za maendeleo,"alisema Bw.  Manasseh.

Kwa upande wake, Kaimu Katibu Tawala Mkoa wa Mtwara, Bw. Abdillah Mfinanga alisema kuwa Wizara hiyo inaendesha mafunzo kwa watendaji wa Serikali waliopo katika ngazi za mikoa, halmashauri, majiji, miji na wilaya kufuatia kuwepo kwa changamoto mbalimbali zinazohusu utekelezaji wa Sheria hiyo.

Aidha mada zilizowasilishwa katika mafunzo hayo ni pomoja na utekelezaji wa Sheria ya Ununuzi wa Umma lenye lengo la kuwafahamisha watanzania juu ya fursa mbalimbali zinazopatikana katika sheria hiyo.


Wananchi wa Wilaya ya Longido Mkoani Arusha wameiomba serikali kujengea uzio shule zote za serikali za bweni zilizopo katika wilaya hiyo lengo ni kuimarisha ulinzi na kuthibiti vitendo vya uchomaji moto mabweni vinavyokithili katika wilaya hiyo.

Agosti 26 mwaka huu bweni moja la shule ya sekondari mchanganyiko ya Enduiment iliyopo Kijiji cha Lerangwa Kata ya Olmology Tarafa ya Enduiment wilayani humo liliungua moto na septemba mosi mwaka huu bweni lingine moja tena liliungua moto na kufanya wazazi wa wanafunzi hao kuwa na wasiwasi na Maisha ya watoto wao wakiwa shule.

Mmoja wa Mzazi wa Wanafunzi hao aliyejitambulisha mbele ya Naibu Waziri wa Madini na Mbunge wa Longido,Dkt Steven Kiruswa aliyekwenda tena shuleni hapo kuangalia uhalibifu huo wa Moto uliochoma bweni hilo,Oliver Pallangyo alisema alisema shule hiyo haina uzio hivyo ni wakati wa shule zote za bweni Longido kuwekwa uzio na kuwa na walinzi ili kulinda mali za shule na wanafunzi.

Pallangyo alisema vitendo vya uchomaji moto mabweni ya wanafunzi vinapaswa kuthibitiwa na wahusika wanapaswa kusakwa na kuchukuliwa hatua kwani leo inaweza kuwa hapa na kesho inaweza kuwa sehemu nyingine hivyo ni wakati wa kujengea uzio wa umeme kwa shule zote Longido ili wanafunzi waweze kusoma kwa amani.

Alisema na kumshukuru Mbunge Kiruswa kwa kuendelea kutoa misaada kwa wanafunzi hao na wamemwomba Mbunge huyo kutochoka na kuhimiza uongozi wa serikali wilaya ya Longido na serikali Kuu kuangalia hilo la uzio ili wazazi wasiwe na wasiwasi wanafunzi wakiwa shuleni.

Naye Mtawa{Sister}wa Kanisa Katoliki Jimbo Kuu la Arusha,Sister Bertha Shirima yeye aliunga mkono wazo la wazazi wenzake waliotangulia na kusisitiza kuwa hilo ni wazo jema ambalo linapaswa kufanyiwa kazi na serikali kwa kushirikiana na Mbunge wa Jimbo la Longido ili wanafunzi waweze kuzingatia masomo wakiwa shule.

Shirima alisema uthibiti wa uchomwaji moto shule za bweni Longido unapaswa kuimarishwa kwa sasa na wahusika wanapaswa kusakwa usiku na mchana ili hatua zichukuliwe dhidi yao kwani hawana lengo zuri kwa longido na nchi kwa ujumla.

Naye Mjumbe wa Mkutano Mkuu wa CCM na Baraza la Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi {UVCCM} Mkoa wa Arusha,Tezra Furaha pamoja na kuunga mkono wazo la uzio pia alitoa msaada wa magodoro 50 na mablanketi 50 kwa shule hiyo huku akisisitiza kuwa na ushirikiano na Mbunge Kiruswa katika kuleta maendeleo kwa wananchi wa Longido.

Alisema Mbunge Kiruswa ni Mbunge wa mfano katika Mkoa wa Arusha kwani ni Mbunge mwenye kutatua changamoto za wananchi wake kwa haraka na mwenye kujali hivyo anapaswa kuungwa mkono kwa hali na mali hivyo wanapaswa kumlinda kwa gharama yoyote.

Naye Kiruswa mbali ya kutoa magodoro kwa wanafunzi wote 485 na blanket ya idadi hiyo hiyo alisisitiza kupata taarifa sahihi ya wale wanaoihujumu shule hiyo kwa kuchoma moto ili hatua ziweze kuchukuliwa kwa haraka.

Alisema serikali iko tayari kujenga Miundombinu ya shule hiyo lakini kwanza inataka kupata ushirikiano wa kutosha kwa kuwataja wale wote wanaofanya hujumu ya uchomaji moto shule hiyo ili serikali isiweze kupata hasara pindi inapojenga Miundombinu.

‘’Leo hapa sitoki hadi mje muninong’oneze kwa siri akina nani wanahujumu shule kwa kuchoma moto mabweni ili hatua zichukuliwe maana serikali ikijenga halafu wahuni wanachoma itakuwa kazi bure hivyo wahusika wanapaswa kujulikana’’ alisema Kiruswa

Waziri huyo alisema kuwa Waziri wa Elimu ,Professa Aldof Mkenda ametoa fedha taslimu shilingi milioni moja ili ziweze kununuwa magodoro na baadhi ya wabunge wameahidi kuchangia ununuaji wa magodoro na blanketi ili wanafunzi watakaporudi shuleni kila kitu kiwe sawa kwa ajili ya kuendelea na masomo.

Awali bweni moja liliteketea kwa moto n abweni hilo lilikuwa likichukua wanafunzi 340,vitanda 170 na magodoro 340 mali zote zimeteketea kwa moto lakini hakukuwa na maafa.

Afisa Elimu Sekondari Wilaya ya Longido,Gilbert Sombe alisema shule hiyo inahitajika kujengwa mabweni matatu kwa gharama shilingi milioni 390,vitanda 170 vinapaswa kununuwa kwa gharama ya shilingi milioni 142 na magodoro 340 yanapaswa kununuliwa kwa gharama ya shilingi milioni milioni 60.



 Naibu Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Bara, John Mongella, leo Septemba 6, 2024, amekutana na wajumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM Wilaya ya Shinyanga mjini, wajumbe wa baraza la jumuiya, na mabalozi katika ukumbi wa CCM Wilaya ya Shinyanga mjini.


Mkutano huo ulihudhuriwa na viongozi mbalimbali wa CCM pamoja na viongozi wa serikali, akiwemo wakuu wa idara wa Manispaa ya Shinyanga.

Mongella ameanza ziara ya siku saba mkoani Shinyanga kwa lengo la kukagua utekelezaji wa Ilani ya CCM ya 2020-2024 na kuimarisha uhai wa chama. Katika ziara hiyo, atafanya mikutano ya hadhara na ya ndani ili kusikiliza changamoto zinazowakabili wananchi wa mkoa wa Shinyanga.

Ziara hiyo itamfikisha katika maeneo ya Shinyanga Vijijini, Kahama, Msalala, Kishapu, na Ushetu, ambako atakutana na viongozi wa chama na wananchi kujadili namna bora ya kuimarisha utekelezaji wa sera za chama kwa maendeleo ya mkoa.

Pia, ziara hii inalenga kuwahamasisha wanachama wa CCM kushiriki kikamilifu katika shughuli za chama na kushughulikia kero za wananchi.










 


Na. Saidina Msangi, Chalinze, Pwani.


Wananchi wa Halmashauri ya Wilaya ya Chalinze wameishukuru Serikali kwa kuwafikishia elimu ya fedha itakayowasaidia kujikwamua kiuchumi kwa kutumia fursa za uwekezaji ili kujiongezea kipato na kuongeza thamani ya akiba zao.

Wananchi hao walitoa shukrani hizo baada ya kupata mafunzo ya elimu ya fedha yaliyoratibiwa na Wizara ya Fedha, yenye kauli mbiu "Elimu ya fedha ni msingi wa maendeleo ya kiuchumi" ambayo yametolewa kwa siku mbili katika ukumbi wa mikutano wa Wilaya ya Halmashauri ya Chalinze.

                                                  
Akizungumza kwa niaba ya washiriki wenzake, Bi. Mery Leonard Chiwiko, aliishukuru Wizara ya Fedha kwa kuwapa elimu hiyo muhimu, akisema kuwa hapo awali hawakuwa na uelewa mzuri kuhusu masuala ya fedha, mikopo na uwekezaji.


"Tunaishukuru Wizara ya Fedha kwa kutupatia elimu hii, itatusaidia sana katika kuimarisha maisha yetu ya kifedha, kuepukana na mikopo umiza na pia tumejifunza kuwa hata kama una kipato kidogo inawezekana kuweka akiba na kuwekeza akiba hiyo na kupata faida," alisema Chiwiko.


Wananchi hao waliiomba Serikali kuona namna ya kuwafikishia mafunzo ya elimu ya fedha ikiwezekana mara mbili kwa mwaka kutokana na umuhimu wake katika kuwawezesha kukabiliana na changamoto za kiuchumi.


Timu ya Maafisa kutoka kutoka Wizara ya Fedha imetoa mafunzo ya elimu ya fedha ikiwemo namna ya kuweka akiba na mbinu za usimamizi wa fedha na uwekezaji kwa washiriki zaidi ya 800 ambao wanatarajiwa kuwa mabalozi wa kuwafikishia wenzao elimu hiyo ili nao waweze kunufaika na kujikwamua kiuchumi.


 


KATIBU wa NEC, Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa CCM Taifa, CPA Amos Makalla, amesema Ngorongoro ni ngome ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) na hakuna chama mbadala kitakacho watatulia kero wananchi wa eneo hilo.

CPA Makalla, ameyasema hayo  kwenye mkutano wa hadhara wa CCM uliofanyika katika Uwanja wa Mazingira Bora, ikiwa ni muendelezo wa ziara yake ya siku 6 katika Wilaya ya Karatu, Longido, Monduli.

Amesema, baada ya mrejesho aliopata baada ya kikao cha ndani alichofanya na baraza la madiwani na wajumbe wa Kamati ya siasa Ngorongoro, ambapo wajumbe hao wameeleza kuonesha kuridhishwa na mwenendo wa CCM huku wakidai kuendelea kuunga mkono juhudi za Mwenyekiti wa CCM na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan.

Pia CPA Makalla amesema, kutokana na Maendeleo yanayofanywa na Serikali ya CCM wananchi wa Ngorongoro kupitia viongozi hao, wameahidi kuendelea kukiunga mkono chama cha CCM na kusema kuwa hakuna chama mbadala kitakachoweza kuwaletea maendeleo.

Aidha, CPA Makalla amesema kuwa, mbali na kutoweza kufika Wilaya ya Ngorongoro kutokana na zuio la Jeshi la Polisi lililotolewa hivi karibuni, amesema bado CCM inatambua mchango wa wakazi wa eneo hilo na kuahidi kuendelea kupeleka maendeleo na chama hicho kitajitahidi kufika pindi watakaporuhusiwa.

 


Na. Joseph Mahumi na Peter Haule, WF, Dodoma


Serikali imesema inaendelea kuweka mikakati na mbinu mbalimbali za muda mfupi, wa kati na mrefu katika kushughulikia changamoto ya uhaba wa Fedha za Kigeni (Forex), ikiwemo kuainisha baadhi ya sekta ambazo zinaweza kuleta mapato zaidi ambayo yatatoa suluhisho la kudumu la uhaba wa fedha za kigeni.

Hayo yamesemwa na Waziri wa Fedha, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb), wakati alipokutana na kufanya mazungumzo na Balozi mpya wa Uingereza nchini Tanzania, Mhe. Marrianne Young aliyefika Ofisini kwake Jijini Dodoma kwa ajili ya kujitambulisha.

Mhe. Dkt. Nchemba amesema kuwa, katika bajeti inayoendelea, Serikali imeweka vipaumbele kwa baadhi ya sekta ambazo ni za kuongeza mapato ya fedha za kigeni japokuwa kama nchi kuna hali tofauti na baadhi ya nchi nyingine zinazoizunguka Tanzania kwakuwa inatekeleza miradi mikubwa ya kimkakati.

Aliongeza kuwa, hali hiyo imesababishwa na kutokuwa na uwiano katika uingizaji wa bidhaa nchini na uuzaji wa bidhaa nje ya nchi, lakini pia imetokana na utekelezaji wa miradi mbalimbali ya kimkakati kama mradi wa kuzalisha umeme wa Bwawa la Nyerere, mradi wa Reli ya Kisasa (SGR) na Daraja la Busisi.

“Ni wazi kwamba kila unapokuwa na tofauti yoyote kati ya kile unachouza nje na kile unachoagiza kutoka nje, kutakuwa na shinikizo kwenye fedha za kigeni, na hicho ndicho kinachotokea na pia mikakati na hatua zinazochukuliwa zitasaidia kupata suluhisho la kudumu siku za karibuni” alisema Mhe. Dkt. Nchemba.

Aidha Mhe. Dkt. Nchemba alitumia fursa hiyo kumpongeza Balozi huyo kwa kuteuliwa kuwa Balozi wa Uingereza nchini na kuahidi kuendelea kufanya kazi pamoja ili kuendeleza ushirikiano kati ya Tanzania na Uingereza katika kuhakikisha maendeleo endelevu ya kiuchumi. 

“Dhamira ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania chini ya Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ni kuendelea kushirikiana na Serikali ya Uingereza ili kuimarisha ushirikiano muhimu wa maendeleo” alisema Dkt. Nchemba.

Mhe. Dkt. Nchemba aliongeza kuwa, Uingereza ni mdau muhimu wa maendeleo kwa kuendelea kutekeleza ajenda ya Maendeleo ya Kitaifa kama ilivyoainishwa chini ya Dira ya Maendeleo ya Taifa 2025 na Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano 2021/22–2025/26 (FYDP III).

“Tunashukuru sana kwa msaada thabiti ambao Serikali ya Uingereza imekuwa ikitoa kwa Tanzania, hususan katika maeneo ya ulinzi wa kijamii kupitia Mpango wa TASAF awamu ya II, Sekta ya Elimu, Afya kupitia Mfuko wa Pamoja wa Afya na Msaada wa Mpango wa Kupambana na Rushwa ambao umechangia kwa kiasi kikubwa maendeleo endelevu ya kiuchumi nchini Tanzania” alisema Dkt. Nchemba.

Kwa Upande wake, Balozi huyo mpya wa Uingereza nchini, Mhe. Marrianne Young, amemshukuru Waziri wa Fedha, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba Madelu kwa kumkaribisha na kuahidi kuendeleza ushirikiano kati yao katika kusukumu gurudumu la maendeleo ya kiuchumi kwa Tanzania.

“Ningependa kuwapongeza kwa sera imara za uchumi wa jumla na maendeleo, Ninaelewa kwamba tumekuwa na msaada wa muda mrefu kutoka Mamlaka ya Mapato na Forodha ya Uingereza (HMRC) katika eneo hili na tunafanya kazi zaidi ili kusaidia juhudi za Serikali ya Tanzania za kuongeza wigo wa mapato”

Kikao hicho kimehudhuriwa na Kamishna wa Idara ya Usimamizi wa Madeni Wizara ya Fedha, Bw. Japhet Justine, viongozi wandamizi wa Wizara ya Fedha na Maafisa kutoka Ubalozi wa Uingereza.