Katika kuhakikisha wakulima wa tumbaku wanapata ruzuku za mbolea Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA), Bw. Joel Laurent, amefanya ziara ya kikazi katika vituo viwili vinavyo hakiki taarifa hizo mkoani Tabora kujionea maendeleo ya zoezi hilo na kuhakikisha linakamilika kwa wakati.
Baada ya kutembelea vituo hivyo katika ofisi za Chama Kikuu cha Ushirika Mirambo na ofisi za Chama Kikuu cha Ushirika wa Wakulima wa Tumbaku Kanda ya Magharibi (WETCU), Bw. Laurent amesema kuwa, zoezi hilo limefikia hatua nzuri itakayowezesha kuanza kwa taratibu za malipo kwa wakulima wa Tumbaku nchini.
Akizungumza wakati wa ziara hiyo, Bw. Laurent ameeleza kuwa, lengo la uhakiki ni kuhakikisha wakulima wote waliozalisha Tumbaku katika msimu wa mwaka 2023/2024 wanalipwa na fedha hizo zinamfikia mkulima anayestahili moja kwa moja kupitia akaunti yake.
Ameeleza kuwa, zoezi hili linafanyika kwa ushirikiano kati ya Wizara ya Kilimo, TFRA, TCDC na vyama vikuu vya ushirika vilivyo chini ya shirikisho la TCJE.
Akizungumza na Mkurugenzi Laurent, Ndg. Innocent Nsena Katibu Tawala wa Wilaya ya Urambo alieleza kuwa, suala la ruzuku limekuwa kilio cha muda mrefu kutoka kwa wakulima na kwamba utekelezaji wa mpango huu utapunguza gharama za uzalishaji kwa mkulima.
“Ninamshukuru Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kuridhia ombi la kutoa ruzuku kwa wakulima wa tumbaku, kwa kuwa zao hili awali halikuwa miongoni mwa mazao yanayopata ruzuku” alisema Ndg. Nsena.
Kwa upande mwingine, akitoa taarifa ya utekelezaji wa zoezi la uhakiki katika ofisi za Chama Kikuu cha Ushirika WETCU, kiongozi wa timu hiyo, Ndg. Byaga Nzohumpa, alieleza kuwa, zoezi hilo limekamilika kwa asilimia 100 baada ya kuhakiki taarifa za vyama vya msingi 248 walivyokabidhiwa.
Naye Ndg. Godwin Mwalongo, kiongozi wa timu ya uhakiki katika ofisi za Chama Kikuu cha Ushirika Mirambo, amesema kuwa, kazi ya uhakiki imefikia hatua nzuri na inatarajiwa kukamilika kwa wakati.
Kwa upande wake, Kaimu Meneja wa TCJE, Ndg. Seleman Abasi Maona, alieleza kuwa, miongoni mwa changamoto kubwa zilizokabili zoezi hilo ni uandaaji hafifu wa takwimu za wakulima wa tumbaku kwa msimu wa kilimo wa 2023/2024, hasa kutokana na taarifa zisizo sahihi kutoka kwa wakulima.
Alisisitiza kuwa kama kungekuwepo mfumo madhubuti wa ukusanyaji taarifa kuanzia ngazi ya chini, changamoto hizo zingeweza kuepukwa na kuahidi kuboresha kwa ajili ya manufaa ya baadaye kwa wakulima.
Post A Comment: