Na. Josephine Majura na Chedaiwe Msuya, WF, Dodoma
Serikali kupitia Wizara ya Fedha imefanya kikao kazi cha mapitio ya Matumizi ya Fedha za Umma ngazi ya Sekta (Public Expenditure Review -PER) katika Sekta mbalimbali zinazoshirikiana katika utekelezaji wa bajeti ya Serikali ikiwemo Sekta ya Kilimo, Maji, Elimu, na Afya ili kuongeza tija, uwazi, na uwajibikaji katika Matumizi ya Fedha za Umma.
Akifungua kikao kazi hicho, Mkurugenzi wa Utawala na Usimamizi wa Rasilimali Watu, Wizara ya Fedha, Bw. Lusius Mwenda, amesema kuwa Serikali ina wajibu wa kufanya Mapitio ya Matumizi ya Fedha za Umma (PER) kila mwaka wa fedha kwa mujibu wa Sheria ya Bajeti ya Mwaka 2015.
Alifafanua kuwa lengo la kikao kazi hicho ni kuhakikisha fedha za umma zinatumika kwa ufanisi, kutambua changamoto na fursa zilizopo katika utekelezaji wa bajeti, kuimarisha ushirikiano wa kisekta katika mipango ya Serikali na kutoa mapendekezo yatakayosaidia kusimamia na kutekeleza Mpango na Bajeti kwa ufanisi zaidi.
“Mapitio ya Matumizi ya Fedha za Umma si zoezi geni, kwani hadi mwaka 2016 yalifanyika kwa kushirikiana na wadau wa maendeleo ikiwemo Benki ya Dunia, Shirika la Maendeleo la Watoto na Mashirika yasiyo ya kiserikali, alisema Bw. Mwenda.
Aliongeza kuwa Serikali inaendelea kuthamini mchango wa wadau mbalimbali na itaendelea kuwashirikisha katika midahalo na tafiti za kitaalam kwenye ngazi zote ili kubaini vyanzo vipya vya mapato, kusimamia matumizi ya fedha za umma, na kukuza uchumi kwa ujumla.
Aidha, Bw. Mwenda alisema kuwa ili kuhakikisha zoezi hilo linakuwa na tija zaidi na endelevu, Serikali imeamua kulisimamia zoezi hilo pasipo kutegemea moja kwa moja wadau wengine, ili kuwezesha kusimamia kikamilifu michakato yote ya mapato na matumizi ya fedha za umma.
Kikao kazi hicho kimewashirikisha wataalamu kutoka serikalini na wadau mbalimbali ikiwemo, Hakielimu, Chama cha Biashara, Viwanda na Kilimo Tanzania, Jukwaa la Sera na Taasisi ya kupunguza Umasikini.
Post A Comment: