Na WAF Dodoma.
Menejimenti ya Wizara ya Afya ikiongozwa na Katibu Mkuu Dkt. Seif Shekalaghe, leo Aprili 11 2025 imekagua ujenzi wa jengo la ofisi za Wizara ya Afya lililopo katika Mji wa Serikali Mtumba.
Taarifa ya Mshauri Elekezi ambaye ni Wakala wa Majengo Tanzania (TBA) imebainisha kuwa hatua za ujenzi wa jengo hilo zimefikia asilimia 92 huku Mkandarasi Nadhra Engineering & Company Ltd akiahidi kukamilisha kazi hiyo ifikapo June 30, 2025.
Dkt. Shekalaghe amemtaka mkandarasi kukamilisha kazi kwa wakati na hakutakuwa tena na muda wa ziada wa kuongezewa ili kukamilisha ujenzi.
“Mradi huu umechukua muda mrefu, nataka ujenzi ukamilike ndani ya muda huu kulingana na maazimio tuliyokubaliana hapa ‘site’ baina ya menejimenti ya Wizara na Mkandarasi,” amesisitiza Dkt. Shekalaghe.
Ujenzi wa jengo la Wizara ya Afya hadi kukamilika kwake utagharimu zaidi ya Shilingi Bilioni 26.6 ambapo kukamilika kwa jengo hili kutawezesha watumishi wote wa Wizara ya Afya makao makuu kufanya kazi katika eneo moja hivyo kuleta ufanisi zaidi wa huduma zinazotolewa.
Jengo hili lina mita za mraba 14,355 likijumuisha sakafu kumi (10) mbili zikiwa ni sakafu za ardhini (basement), jengo litakuwa na ofisi zaidi ya 188 pamoja na kumbi za mikutano 13.
Post A Comment: