WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema shilingi trilioni 3.5 zimetolewa na mifuko ya uwezeshaji wananchi kiuchumi iliyopo nchini kwa wanufaika zaidi ya milioni 24 ambapo kati yao, wanawake ni zaidi ya milioni 11 na wanaume ni milioni 13.
“Uanzishwaji wa mifuko na programu za uwezeshaji wananchi unatokana na mahitaji ya kiuchumi kwa maendeleo ya nchi yetu. Mifuko iliyopo imeweza kutoa jumla ya shilingi trilioni 3.5 kwa wanufaika zaidi ya milioni 24,” amesema.
Ameyasema hayo leo (Jumanne, Aprili 15, 2025) Bungeni jijini Dodoma, wakati akitoa hoja ya kuhitimisha mjadala wa bajeti ya Ofisi ya Waziri Mkuu, Taasisi zake na Mfuko wa Bunge kwa mwaka 2025/2026.
Akielezea mambo yaliyofanyika ndani ya miaka minne ya Serikali ya awamu ya sita, inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, Waziri Mkuu amesema serikali imeboresha sera na sheria mbalimbali ili kuwawezesha wananchi kiuchumi.
“Sera na sheria hizo zimewezesha kutenga asilimia 30 ya manunuzi ya umma kwa wanawake, vijana, wazee na watu wenye ulemavu; kuratibu na kuweka mazingira bora kwa vikundi na huduma ndogo za kifedha; pamoja na kuongeza ushiriki wa Watanzania katika uwekezaji ikiwemo sekta za madini, mafuta na gesi.
Waziri Mkuu amesema mifuko na programu za uwezeshaji wananchi zinazoratibiwa na Serikali zinatoa fursa ya mikopo kwa riba nafuu kwa mtu mmoja mmoja na vikundi vya uzalishaji mali. “Serikali itaendelea kutekeleza na kusimamia mikakati ya kutoa elimu kwa wananchi kupitia njia mbalimbali ikiwemo maonesho, makala, vyombo vya habari na vituo vya uwezeshaji ili kuongeza uelewa kuhusu fursa zilizopo kwenye mifuko na programu hizo,” amesema.
Ameitaja baadhi ya mifuko na programu hizo kuwa ni Mpango wa Mikopo ya Halmashauri wa asilimia 10 kwa Wanawake, Vijana na Wenye Ulemavu; Programu ya Jenga Kesho Iliyo Bora (BBT); Programu ya Taifa ya Kukuza Ujuzi kwa Vijana; Programu ya Kukuza Viwanda Vidogo na vya Kati; Programu ya Imarisha Uchumi na Mama Samia (IMASA); na Mfuko wa Dhamana wa Wajasiriamali Wadogo.
Wakati huohuo, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu), William Lukuvi amesema ujenzi wa Kiwanda cha Uchapishaji wa nyaraka za Serikali Dodoma unafanyika kwa awamu ambapo awamu ya kwanza ilihusisha ujenzi wa Jengo la Kiwanda ambao ujenzi wake umekamilika.
“Awamu ya pili inahusisha ujenzi wa jengo la utawala, uzio na kazi za nje ambao umefikia asilimia 40. Aidha, Kazi ya usimikaji mashine mpya nane za uchapishaji inaendelea na inatarajiwa kukamilika na kuanza kazi mwezi Mei, 2025 ili kuhakikisha Idara ya Mpigachapa ya Serikali inatekeleza majukumu yake,” amesema.
Ametoa kauli hiyo leo jioni wakati akichangia hoja ya Waziri Mkuu wakati wa kuhitimisha majadiliano ya makadirio ya mapato na matumizi ya fedha kwa mwaka wa fedha 2025/2026.
Alikuwa akijibu hoja iliyotaka Serikali ihakikishe kwamba ujenzi wa Kiwanda cha Uchapishaji wa Nyaraka za Serikali unakamilika kwa wakati na mashine za uchapaji zinasimikwa kwa wakati ili kuwezesha Kiwanda kutekeleza majukumu yake.
Kwa mwaka 2025/2026, Bunge limeidhinisha sh. 595,291,624,000/- ambapo kati ya fedha hizo, sh. 183,821,010,000/- ni kwa ajili ya matumizi ya kawaida na sh. 411,470,614,000/- ni kwa ajili ya matumizi ya maendeleo kwa Ofisi ya Waziri Mkuu na taasisi zilizo chini yake.
Vilevile, Bunge limeidhinisha sh. 186,793,635,000/- kwa ajili ya Mfuko wa Bunge. Kati ya fedha hizo, shilingi 174,960,303,000 ni kwa ajili ya matumizi ya kawaida na shilingi 11,793,332,000 ni kwa ajili ajili ya matumizi ya maendeleo.
(mwisho)
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
S. L. P. 980,
DODOMA.
JUMANNE, APRILI 15, 2025.
Post A Comment: