Katika hatua ya kuimarisha sekta ya madini na kuwawezesha wachimbaji wadogo nchini kunufaika zaidi na rasilimali za madini, Waziri wa Madini, Mhe. Anthony Mavunde, ameteua timu maalum ya wataalam kutoka Serikalini na sekta binafsi kwa ajili ya kuishauri Wizara ya Madini namna bora ya kuwainua wachimbaji hao kiuchumi kupitia uchimbaji wenye tija.

Akizungumza jijini Dodoma leo Aprili 9, 2025, Waziri Mavunde amesema timu hiyo ni sehemu ya utekelezaji wa maelekezo ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, aliyetoa wito kwa Wizara kuhakikisha sekta ya madini inapiga hatua huku wachimbaji wadogo wakichimba kwa tija na manufaa makubwa zaidi na hivyo kuwajenga kiuchumi zaidi.

“Kutokana na umuhimu wa Sekta hii ndogo ya uchimbaji madini mdogo, naomba nitumie nafasi hii kuwakumbusha kuwa, Sera yetu ya Madini ya Mwaka 2009 imeweka bayana kuwa, mkakati wetu ni kuwaendeleza wachimbaji wadogo wa madini kwa kuhakikisha wanaendesha shughuli zao kisasa sambamba na kuhakikisha wanakuwa na taarifa za kutosha za kijiolojia katika maeneo yao ya uchimbaji, kukuza mitaji yao, utaalamu pamoja na utunzaji wa mazingira.

Ilani ya Chama cha Mapinduzi (CCM) imeweka dhamira ya kuongeza fursa za ajira kwa Watanzania kupitia Sekta mbalimbali ambapo madini ni mojawapo na kwamba Serikali kupitia Wizara ya Madini inakila sababu ya kuhakikisha kuwa, Sekta ya uchimbaji mdogo wa madini inaendelea kukuwa na inatoa fursa ya ajira kwa Watanzania. 

“Ili sekta ya madini ikue kwa kasi na tija zaidi, ni lazima tuwape nafasi kubwa Watanzania katika kushiriki moja kwa moja kwenye uchumi huu. Hii timu tumeiunda mahsusi kwa ajili ya kuhakikisha wachimbaji wadogo wanapata msaada wa kitaalam, mitaji, maeneo ya uchimbaji na teknolojia ya kisasa na kuweka mfumo mzuri wa kusaidia kutoka uchimbaji mdogo,kati mpaka mkubwa”Alisema Mavunde

Ametaja Hadidu za rejea kwa timu Timu hiyo kuwa ni amoja na Kupendekeza namna bora za kuwawezesha wachimbaji wadogo kiuchumi kupitia uchimbaji wenye tija. Kutoa mapendekezo na kuendeleza wazo la kuundwa kwa Benki ya Wachimbaji Wadogo pamoja na Kupendekeza njia bora za kuanzishwa kwa Mfuko wa Madini kwa ajili ya kuwawezesha wachimbaji wazawa.

Timu hiyo itaongozwa na Mwenyekiti Victor Tesha (Makamu wa Rais, FEMATA), Katibu akiwa ni Dkt.Abdulrahman Mwanga (Kamishna wa Madini) huku Wajumbe wakiwa ni Theobald Sabi (Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya NBC,Mwenyekiti wa Mabenki na Taasisi za Fedha), Ivan (Mtaalam wa Masuala ya Kifedha), Dkt. Mussa Budeba (Mkurugenzi Mtendaji wa GST), Hadija Ramadhani (Mwanasheria kutoka Tume ya Madini) na Dkt. Theresia Numbi (Mwanasheria na Mtaalam wa Local Content)

Timu hiyo imepewa muda wa mwezi mmoja kuwasilisha mapendekezo yake rasmi kwa Wizara, ambapo Waziri Mavunde amesisitiza kuwa serikali iko tayari kuyafanyia kazi mapendekezo hayo mara moja kwa lengo la kuongeza mchango wa wachimbaji wadogo katika pato la taifa.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Timu, Ndg. Victor Tesha amesisitiza kuwa wanaenda kufanya kazi hiyo kwa uaminifu na weledi mkubwa ili kulinda imani ya se kwa kuzingatia taaluma na uzoefu.







Share To:

Post A Comment: