Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Mhandisi Hamad Yussuf Masauni amezindua Bodi ya tisa ya Baraza la Taifa la Uhifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) ikiwa pamoja na kuipa meno katika utekelezaji wa majukumu yake.

Bodi hiyo imezinduliwa Dodoma Aprili 15, 2025, ambapo Mhandisi Mwanasha Tumbo ndiye Mwenyekiti wa Bodi hiyo huku katika kuisaidia Bodi hiyo kutekeleza vyema majukumu yake ya msingi, pamoja na kuliwezesha Baraza kutekeleza majukumu Waziri Masauni ameielekeza mambo mbalimbali yatakayosaidia utekelezaji ili kufanikisha malengo.

Waziri Masauni amesema Bodi inapaswa kushirikiana kwa karibu na Menejimenti ya Baraza ili kuleta matokeo yenye tija, Kusimamia vizuri Baraza ili kudhibiti uchafuzi wa mazingira nchini.

Pia Bodi imepaswa kuhamasishaji na kutoa elimu kwa umma kuhusu umuhimu wa kuhifadhi mazingira sababu bado Wananchi hawana elimu ya kutosha kuhusu umuhimu wa kuhifadhi mazingira, hivyo hushiriki katika shughuli zinazochangia uharibifu wa mazingira kama ukataji miti hovyo, uchomaji misitu, na utupaji taka ovyo.

“Ushirikiana na Wizara pamoja na Baraza katika mchakato wa marekebisho ya Sheria ya Usimamizi wa Mazingira, Sura 191 ambao umelenga kuliimarisha Baraza katika usimamizi wa mazingira nchini.

“Bodi kuendelea kubuni na kuandaa mikakati ya Kukabiliana na Mabadiliko ya tabianchi kama ilichambuliwa katika Mikataba ya Kimataifa katika eneo hilo kwani kuongezeka kwa joto duniani, kupungua kwa mvua au mvua zisizotabirika, na majanga kama mafuriko au ukame vinachangia kuharibu mazingira na rasilimali za asili,” amesema Waziri Masauni.

Ameongeza kuwa ukuaji wa haraka wa miji (urbanization) bila mipango bora ya matumizi ya ardhi, hali inayosababisha msongamano, uchafuzi wa mazingira, ukosefu wa mifumo ya maji safi na taka, na uharibifu wa vyanzo vya maji na kingo za mito na bahari

Amesisitiza kuwa Bodi inapaswa kufanya vikao vya kawaida ambavyo ni kwa mujibu wa Sheria na kuhakikisha Menejimenti inawasilisha taarifa za utendaji kwa wakati ili ziidhinishwe na Bodi na kuwasilishwa kwenye Mamlaka husika za Serikali.

Waziri Masauni ameielekeza Bodi kusimamia mapato na matumizi ya Baraza na kuhakikisha matumizi ya Mifumo ya Kieleketroniki katika ukusanyaji wa Mapato ya Baraza. Aidha, ni vema pia Bodi hii iangalie namna ya kuliwezesha Baraza kupata watumishi wa kutosha ili kuliwezesha kufikia adhma hii.

Mwisho Bodi inatakiwa kuendelea kutoa miongozo sahihi katika ushughulikiwaji wa malalamiko yanayowasilishwa na wananchi na wadau wengine kuhusu uchafuzi na uharibifu wa mazingira wengine wanaounda Bodi hiyo ni Bi. Kemilembe Mutasa, Dkt. Abubakar Rajab, Prof. Hamis Malebo, Prof. Theobald Theodory, Mha. Bashir Mrindoko, Bw. Said Tunda, Bw. Alex Mgongolwa na Bi. Rabia Hamid.

Share To:

Post A Comment: