Katika kuadhimisha Wiki ya Afya Kitaifa, Kaimu Mkurugenzi wa Huduma za Kinga kutoka Wizara ya Afya Dkt. Otilia Gowelle ametoa wito kwa Watanzania kujenga mazoea ya kufanya mazoezi mara kwa mara na kupima afya  ili kujikinga na magonjwa  Yasiyoambukiza.

Dkt. Gowelle ametoa Wito huo Jijini  Dodoma   leo tarehe 6, Aprili, 2025 katika Matembezi Maalum ya kuhamasisha mazoezi ya viungo katika kuimarisha afya ya mwili ikiwa ni mwendelezo wa wiki ya Afya.

“ Katika kuadhimisha Wiki ya Afya,  Siku ya leo tarehe 6, Aprili, 2025 tumefanya matembezi  katika kujenga afya bora, hivyo nitoe wito kwa watanzania tuendelee kuimarisha  Afya zetu pia tupime na tuchunguze afya zetu mara kwa mara”amesema Dkt. Gowelle.

Aidha, Dkt. Gowelle ametumia fursa hiyo  kuhamasisha  Wakazi wa Dodoma na Mikoa jirani kuendelea kujitokeza katika Kituo cha Mikutano cha CCM Jakaya Kikwete Dodoma kupata huduma mbalimbali za afya ikiwemo upimaji bure pamoja na elimu ya afya.

“Kuna huduma mbalimbali za afya zinaendelea katika mabanda hapa CCM Jakaya Kikwete, niwaombe Wakazi wa Dodoma na mikoa jirani wajitokeze kwa wingi kupima  afya  na huduma hizi bure zinaendelea hadi tarehe 8, Aprili, 2025”amesema.

Issa Ng’imba  ni Mkurugenzi wa Utawala na Usimamizi wa Rasilimali  Watu kutoka Wizara ya Afya  amesema  Wizara itahakikisha kuwa Watumishi wanajumuika na jamii kufanya mazoezi mara mbili kwa mwezi.

“Tutahakikisha kuwa watumishi wote wanajumuika na jamii kufanya mazoezi mara mbili kwa mwezi ili kujenga taifa la watu imara”amesema.

Kwa upande wake Mkurugenzi Msaidizi Magonjwa Yasiyoambukiza, Afya ya Akili na Ajali kutoka Wizara ya Afya Dkt. Omary Ubuguyu amesema  Magonjwa Yasiyoambukiza yameongezeka kwa kiwango Kikubwa  hivyo kufanya mazoezi sehemu ya Kinga na kuiunganisha jamii kuwa  na furaha katika kuzuia magonjwa ya akili.

“Tunafanya mazoezi ili kuwa na furaha, kuondoa msongo wa mawazo na kuzuia magonjwa ya akili”amesema.

Mmoja wa washiriki wa Mazoezi hayo, Bahati Matola  Katibu wa Kikundi cha Wanawake na Samia  amesema  kupitia mazoezi hayo imemsaidia kuimarisha afya huku akisisitiza wananchi wengine hasa wanawake kubadilika na kufanya mazoezi.

“Wanawake Tanzania tufanye mazoezi, mazoezi ni afya, na mazoezi sio wanaume tu”amesema.

Ikumbukwe kuwa, Wiki ya Afya Kitaifa 2025  inakwenda sambamba na kaulimbiu”Tulipotoka, Tulipo, Tunapoelekea, Tunajenga Taifa Imara lenye Afya,ambapo itaendelea hadi tarehe 8, Aprili, 2025 huku huduma mbalimbali za Afya zikitolewa  bure katika Kituo cha Mikutano cha CCM Jakaya Kikwete.



Share To:

Post A Comment: