Na Asia Singano, WF – Zanzibar.
Wataalam wa Ubia kati ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi nchini, wameagizwa kuhakikisha miradi yote mikubwa yenye mvuto wa kibiashara nchini inatekelezwa kwa njia ya Ubia kati ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi (PPP) ili kukuza uchumi wa nchi.
Agizo hilo limetolewa Visiwani Zanzibar na Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya Fedha, Bi Amina Khamis Shaaban, wakati akifunga Kikao cha Pili kuhusu Ushirikiano baina ya Ofisi ya Rais, Kazi, Uchumi na Uwekezaji, Zanzibar na Wizara ya Fedha, Tanzania Bara, katika masuala ya Ubia Kati ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi (PPP), kilichofanyika katika Ukumbi wa ZURA visiwani humo.
Alisema Serikali itaendelea kutoa ushirikiano kwa Sekta Binafsi ili kurahisisha utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo na kuhakikisha wananchi wanapata huduma nzuri katika nyanja mbalimbali ikiwemo afya, elimu na huduma nyingine zote muhimu kwa ubora na urahisi na kukuza uchumi wa nchi.
‘’Ni muhimu kushirikisha sekta binafsi katika mipango ya maendeleo, ambao wao wana ujuzi wana utaalamu lakini vilevile wengine wana fedha kwa hiyo hilo ni jambo muhimu katika kushirikiana nao’’ alisema Bi. Amina.
Kwa upande wake Naibu Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Kazi, Uchumi na Uwekezaji, Zanzibar, Bw. Rashid Ali Salim, ameitaka Sekta Binafsi nchini kutumia fursa zilizopo Serikalini za kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo kwakuwa pande zote mbili zitanufaika na fursa hizo.
‘’Tunaialika Sekta Binafsi kuja kuwekeza katika miradi hii ambayo ina manufaa makubwa mbali na ajira na kulipa kodi, miradi hii hurejeshwa Serikalini baada ya muda tutakaokubaliana kwa mujibu wa mkataba" alisema Bw. Salim.
Naye, Kaimu Kamishna wa Kitengo cha Ubia Kati ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi (PPP), Wizara ya Fedha, Bw. Bashiru Taratibu, alisema Wizara ya Fedha, kupitia Kitengo cha PPP, itaendelea kuungana kwa pamoja na Idara ya PPP Zanzibar, kuendelea kushawishi Sekta Binafsi kushirikiana na Sekta ya Umma kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo.
‘’Ahadi yetu sisi ni kushirikiana na wenzetu hawa kuhakikisha kuwa tunatengeneza mazingira mazuri yatakayowezesha kuvutia sekta binafsi kuja kuungana na Serikali zetu zote mbili kuhakikisha tunatekeleza miradi hii ya maendeleo’’ alisema Bw. Taratibu.
Hiki ni kikao cha Pili cha mashirikiano kati ya Ofisi ya Rais, Kazi, Uchumi na Uwekezaji, Serikali ya Mapinduzi Zanzibar na Wizara ya Fedha, Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ambapo Kikao cha kwanza kilifanyika Desemba mwaka wa fedha 2024/2025, huku Kikao kinachofuata kikitarajiwa kufanyika mwaka ujao wa fedha
Post A Comment: