Na FARIDA MANGUBE, MOROGORO


Wananchi wa Kijiji na Kata ya Mangae, Tarafa ya Mlali, Wilaya ya Mvomero mkoani Morogoro, wameanza kunufaika na mradi mkubwa wa maji uliotekelezwa na Wakala wa maji safi na usafi wa Mangira Vijijini (RUWASA), wenye thamani ya zaidi ya shilingi milioni 600.

Mradi huo, unatarajiwa kuwahudumia zaidi ya wakazi 4,000, umezinduliwa rasmi na Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa 2025 jambo ambalo limeleta faraja kwa wakazi wa eneo hilo ambao kwa muda mrefu wamekuwa wakikabiliwa na uhaba wa maji safi na salama.

Akizungumza kwa furaha, mmoja wa wananchi wa Kijiji cha Mangae, Bi. Emiliana Costantine alisema wamekuwa wakipata shida kubwa ya huduma ya maji, mara nyingine wakilazimika kutumia maji yasiyo salama na kutembea umbali mrefu kufuata maji ya visima.

"Mradi huu umetusaidia sana, sasa tunapata maji karibu na makazi yetu kupitia mabomba. Tunautumia muda tuliokuwa tukitumia kutafuta maji kufanya shughuli za maendeleo kama kilimo na biashara," alisema Bi. Emiliana.

Meneja wa RUWASA Wilaya ya Mvomero, Mhandisi Nasibu Mlenge, amesema kuwa mradi huo ni sehemu ya jitihada za serikali katika kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora za maji, na kwamba una manufaa kwa wananchi wapatao 4,049.

Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Mvomero, Judith Nguli, amesema Mwenge wa Uhuru mwaka huu utatembelea na kuzindua miradi saba yenye thamani ya jumla ya shilingi bilioni 1.8 katika wilaya hiyo, ikiwa ni sehemu ya kukuza maendeleo ya kijamii na kiuchumi kwa wananchi.

Uzinduzi wa mradi huo wa maji umeleta matumaini mapya kwa wakazi wa Mangae, ambao sasa wanaangalia maisha kwa mtazamo chanya zaidi wakitegemea maendeleo ya haraka kutokana na uwepo wa huduma hiyo muhimu.
Share To:

Post A Comment: