WANANCHI wa kata  nane za Jimbo la Vunjo mkoani Kilimanjaro  wamesifu uwakilishi na utendaji  Kazi wa Mbunge wa Jimbo lao  Dkt Charles Kimei kwa kazi nzuri za miradi ya Maendeleo katika kata zao.

Miongoni mwa kata zilizotoa pongezi hizo ni pamoja na kata za Marangu Mashariki, Njiapanda, Kahe Mashariki, Kirua Vunjo Kusini, Kilema Kusini, Kirua Vunjo Mashariki, Makuyuni na Kirua Vunjo Magharibi.

Wakitoa pongezi hizo kwa nyakati tofauti kwa Mbunge huyo,Mmoja wa wananchi wa Kata ya Marangu Mashariki, Rosemary Mosha  alisema kwa kipindi hiki Mbunge huyo ameonesha tofauti kubwa baina yake na wabunge waliowahi kuongoza katika jimbo lao.

Alisema Mbunge Dkt.Kimei  amekuwa anaonekana   mara kwa mara Jimboni humo na kusikiliza kero pamoja na changamoto za wananchi wake na kuchukua hatua mbalimbali za kuzitatua.

Mosha alisema katika jimbo lao wameweza kupiga hatua kubwa  katika miradi ya miundombinu ya barabara akitolea mfano daraja linalounganisha vijiji vya Sembeti na Samanga, Upanuzi wa daraja la Marangu Mtoni, ujenzi wa kituo cha Afya Marangu Hedikota, miradi ya elimu na maji.

Kwa Upande wake Richard Kawiche kutoka Kata ya Marangu Mashariki alisema Mbunge Kimei amewaletea kiasi cha sh. Milioni 2 kwaajili ya  ujenzi wa maabara shule ya Sekondari Sakayo Mosha, Kiasi cha Shilingi Milioni  1.5 kwaajili  ya ujenzi wa kivuko Mshiri akishirikiana na wadau.

"Mbali na hayo Mbunge wetu Dkt.Kimei  ametuchangia madawati 50  katika  Shule ya Sekondari  ya Ashira na sasa tuna mradi wa Shilingi Milioni 346 wa kuimarisha upatikanaji wa maji safi  katika vijiji vya Samanga na Rauya kupitia Mamlaka ya maji safi na usafi wa mazingira mjini Moshi (Muwsa).

Naye mzee maarufu  wa kata ya Kahe Mashariki,Mzee Hardson Mmanyi alisema wanampongeza  Mbunge huyo pamoja na Rais Dkt.Samia  Suluhu Hassan kwa kazi nzuri na kubwa wanayofanya ya kupeleka Maendeleo katika kata yao. 

Alisema wameona  namna  walivyofanikisha ujenzi wa barabara ya Papliki - Majengo - Kochakindo,kufikisha   umeme katika kijiji cha Kochakindo pamoja na Zahanati inayotoa huduma kwa  hivi sasa mambo ambayo hayakuwepo hapo awali.

"Vunjo lilikua Jimbo la wanasiasa kuja kujipatia ubunge, kuvuna fedha na kutokomea bila uwajibikaji wowote wenye kuacha alama kwenye mahitaji ya wananchi.

" Wabunge wengi walionekana msimu wa uchaguzi hali imekua tofauti kwa Mbunge Dk Kimei amekua anarudi Jimboni na kazi za maendeleo zinaonekana. Nadiriki kusema wanavunjo tumuunge mkono aweze kukamilisha kazi hizi nzuri alizozianza pamoja na Rais Dkt Samia Suluhu Hassan kwa upendo wake kwetu kupitia yeye mwakilishi wetu," Alisema Ally Msangi  kutoka kata ya Makuyuni

Madiwani wa Jimbo la Vunjo wanazungumziaje maendeleo ya Jimbo lao.

Diwani wa Kata ya Makuyuni,  Mhe Dickson Tarimo alisema kata hiyo imepokea miradi mingi ya maendeleo kipindi hiki cha mbunge wa jimbo la Vunjo, Dkt Kimei pamoja na Rais Dkt Samia kwa kazi walizozifanya hawana budi kuwalipa kwa kuwapa kura za kutosha.

Diwani huyo aliainisha kazi mbalimbali alizofanya mbunge huyo katika kata hiyo ikiwemo shule ya Sekondari Himo kujengewa miundombinu ya kidato cha 5&6, kufanikisha kituo cha wagonjwa wa Nje (OPD) Himo kupandishwa hadhi kuwa kituo kamili cha afya na maboresho makubwa ya utoaji wa huduma za afya kwa kukiwezesha kupata dental treatment unit, dental X -Ray, Digital X-Ray, gari jipya la wagonjwa, vifaa na vifaa tiba vya afya ya uzazi, mama na mtoto vya zaidi ya shilingi milioni 74 pamoja na ujenzi wa madarasa na ununuzi wa madawati katika shule zetu za msingi na sekondari. 

Diwani John Kessy wa Kata ya Kirua Vunjo Magharibi aliongeza kuwa  Mbunge Dkt Kimei amefanikisha Kituo cha Afya Kirua Vunjo kilichopo katika kata hiyo kupatiwa fedha shilingi milioni 500 kwa ajili ya upanuzi kwa kujengewa majengo ya maabara, upasuaji, mama na mtoto pamoja na upauaji wa bwalo la shule ya sekondari Pakula na maboresho katika soko lao la Rindima kwa kukamilisha choo cha soko hilo na kufanikisha ujenzi wa paa la soko. 

Naye Diwani  wa Kata ya Njiapanda Mhe Loveness Mfinanga alisema hawamuungi mkono Dkt Kimei kwa sababu ni mwanaCCM mwenzao bali wanamuunga mkono kwa sababu amefanya kazi za maendeleo zinaonekana zinazogusa maisha ya wananchi. 

Akitolea mfano katika kata yake amefanikisha fedha shilingi bilioni 2.3 kujenga mradi wa maji ulioondoa kero ya maji katika kata hiyo kupitia MUWSA, ujenzi wa shule mpya ya sekondari Njiapanda, ujenzi wa zahanati 2 Njiapanda na Pofo, ujenzi wa shule ya msingi Darajani, ukarabati wa shule za msingi Dr Shein na Njiapanda pamoja na matengenezo ya barabara. 

Diwani wa kata ya Kirua Vunjo Mashariki, Mhe Alex Umbela alisema ameshuhudia na kufanya kazi na wabunge wengi lakini Mbunge wa sasa katika jimbo hilo  ni wa kipekee katika utendaji wa matokeo yenye kuonekana.

Akieleza yaliyofanyika kwenye kata yake alisema shule mbili za msingi Mrumeni na Msufini ni kama zimefanyiwa maboresho kwa kujengwa upya, ujenzi wa zahanati mpya ya Kileuo, uboreshaji wa zahanati ya Nganjoni, maboresho soko la Kisomachi na ujenzi wa barabara ya Uchira - Kisomachi - Kolarie kilomita 2.6 kwa kiwango cha lami ambapo mkandarasi wake  hadi sasa yupo. 

Dkt.Kimei alipotafutwa aliwaomba Wana-CCM kuendeleza Umoja ndani ya chama na kuendelea kumsemea vizuri Rais Dkt Samia Suluhu Hassan, Madiwani na CCM ambapo serikali imetekeleza kwa vitendo ahadi zilizotolewa wakati wa uchaguzi mkuu wa mwaka 2020 kupitia ilani ya uchaguzi ya CCM 2020 - 2025.


















Share To:

Post A Comment: