Farida Mangube, Morogoro .

Wakazi wa Wilaya ya Malinyi mkoani Morogoro wameiomba serikali kuboresha miundombinu ya barabara ikiwemo madaraja ili kuwawezesha kufikia masoko kwa urahisi na kuuza mazao yao kwa bei ya soko.

Wakazi hao, ambao wengi wao ni wakulima wa mazao ya biashara na chakula wanasema kukosekana kwa barabara za uhakika kumeendelea kuwafanya wategemee madalali wanaowanunulia mazao kwa bei ya chini.

Wamesema licha ya juhudi kubwa zinazofanywa na Wakala ya Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA)  kuhakikisha barabara za vijijini zinapitika, bado kuna uhitaji mkubwa wa kuboresha barabara zinazounganisha wilaya hiyo na maeneo mengine, ili kukuza uchumi wa wakazi wa Malinyi.

Kauli hiyo imetolewa na wananchi hao wakati wa uzinduzi wa mradi wa ujenzi wa dharura wa kalvati katika barabara ya Lugala–Misegese, iliyopo kijiji cha Lugala, kata ya Igawa. Wananchi wamesifu kazi zinazofanywa na TARURA katika kurudisha mawasiliano na kuboresha miundombinu hususan baada ya athari za mvua kubwa.

Akisoma taarifa ya mradi huo, Meneja wa TARURA Wilaya ya Malinyi  Charles Mang'era alisema kuwa mradi huo umegharimu zaidi ya shilingi milioni 199, ikiwa ni sehemu ya juhudi za serikali kurejesha miundombinu iliyoharibiwa na mvua za El Niño pamoja na Kimbunga Hidaya, zilizotokea kati ya Novemba hadi Mei 2023.

Amesema ujenzi wa kalvati hilo utaongeza uwezo wa miundombinu iliyopo, ambayo ilikuwa inazidiwa na wingi wa maji, na hivyo kusababisha kuvunjika kwa tuta la barabara, kukata mawasiliano na kuathiri shughuli za kiuchumi za watumiaji wa barabara hiyo.

Kwa upande wake, Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru mwaka 2025, Bw. Ismail Ali Ussi, ameipongeza TARURA kwa kazi kubwa wanayoifanya ya kurejesha mawasiliano na kuboresha barabara zilizoharibiwa kutokana na mvua za El Niño na kimbunga Hidaya.

Share To:

Post A Comment: