OR-TAMISEMI
Serikali imelipa madeni ya wakandarasi 457 wa ujenzi na ukarabati wa miundombinu ya barabara waliokuwa wakidai baada ya kutekeleza mikataba yao kwa kiwango kinachostahili malipo.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Mhe. Mohamed Mchengerwa ameyasema hayo jijini Dodoma akifungua semina ya mafunzo elekezi kwa wakandarasi wazawa kuhusu matumizi ya mfumo wa kielektroniki wa 'Samia Infrastructure Portal' unaolenga kuwawezesha kuomba fedha kwa ajili ya kuimarisha mitaji yao katika miradi ya barabara chini ya usimamizi wa Wakala wa Barabara za Mijini na Vijijini (TARURA).
Waziri Mchengerwa amesema hadi kufikia Aprili 9, 2025, wakandarasi hao walikuwa tayari wamelipwa, huku malipo ya wakandarasi wengine 322 yakiwa mbioni kukamilika.
“Hadi kufikia Aprili 11, 2025, Wakandarasi hawa 322 watakuwa wamelipwa na TARURA, maelekezo yangu kwenu TARURA ni kuhakikisha fedha ambazo tayari mmepokea zinagawiwa kwa haraka, kwa usawa na bila upendeleo, watu wapewe haki zao."
“Wakandarasi waliopo katika kanda zote nchini wafikirieni kwa usawa kutokana na kiasi tulichokipokea kutoka Wizara ya Fedha. Keshokutwa mnipe taarifa ya mgawanyo wa fedha hizo kama tulivyokubaliana,”amesema.
Kuhusu semina hiyo maalum ya elimu ya bidhaa ya kifedha iliyoandaliwa kwa ajili ya wakandarasi wazawa, watumishi wa TARURA, na Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Waziri Mchengerwa amesema ni fursa muhimu kwa pande zote kupata uelewa wa kina juu ya utaratibu wa bidhaa lengwa, majukumu ya kila upande, na namna ya kusimamia mchakato huo kwa uwazi na ufanisi.
Awali, Naibu Waziri wa Ofisi ya Rais – TAMISEMI, Mhe. Zainab Katimba amesema kuanzishwa kwa hatifungani ya miundombinu ya Samia ni utekelezaji wa maelekezo ya Waziri Mchengerwa na ni moja ya alama muhimu atakazoziacha katika ofisi hiyo, ikionesha namna alivyotekeleza kwa vitendo dira ya Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kuwekeza katika miundombinu na kuwawezesha wakandarasi wazawa.
Kwa mujibu wa Mkurugenzi wa Idara ya Mikopo wa Benki ya CRDB, Xavery Makwi, amesema hatifungani hiyo ya Samia imewezesha kukusanywa zaidi ya Sh. bilioni 300 ambazo zitawasaidia wakandarasi wazawa kutekeleza kandarasi zao kwa uhakika, tofauti na hali ilivyokuwa hapo awali.
Post A Comment: