OR-TAMISEMI

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, Mhe. Mohamed Mchengerwa, amewataka Wakuu wa Mikoa na Wilaya kote nchini kuhamasisha ushiriki wa wananchi katika Mbio za Mwenge wa Uhuru za mwaka 2025, ambazo zinalenga kuchochea utekelezaji wa miradi ya maendeleo katika halmashauri ili kuboresha utoaji wa huduma kwa wananchi na kuleta maendeleo nchini.

Ametoa agizo hilo akiwa katika Shule ya Msingi Ukombozi, Ikwiriri, kabla ya kumkaribisha Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Taifa, Ismail Ussi, kuzungumza na wananchi waliokusanyika kushuhudia uraghabishaji wa falsafa ya Mwenge wa Uhuru uliofanywa na wanafunzi wa shule hiyo.

Mhe. Mchengerwa amesisitiza kuwa atahakikisha wananchi wanashiriki kikamilifu kwenye maeneo yote ambayo Mwenge wa Uhuru utapita kukagua miradi ya maendeleo na kuwaelekeza Wakuu wa Mikoa, Wakuu wa Wilaya na Wakurugenzi wa Halmashauri kuhakikisha wanahamasisha wananchi kwa nguvu zote kushiriki shughuli hizo muhimu.

“Mbio za Mwenge zinahamasisha maendeleo, na ndio maana zinaambatana na uzinduzi wa miradi ya kimkakati ya maendeleo. Ushiriki wa wananchi ni fursa muhimu ya kuwajengea uelewa katika usimamizi na utekelezaji wa miradi hiyo,” amesema Waziri Mchengerwa.

Aidha, Waziri Mchengerwa amemweleza Kiongozi wa Mbio za Mwenge Taifa, kuwa Wilaya ya Rufiji imepiga hatua kubwa katika miradi ya maendeleo ikiwemo ujenzi wa shule, barabara, masoko, vituo vya afya na zahanati, miradi ambayo baadhi yake itakaguliwa na Mwenge wa Uhuru mwaka huu.

Kwa upande wake,  Ismail Ussi amesema kila Mtanzania anapaswa kuienzi falsafa ya Baba wa Taifa, akisisitiza kuwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ameendeleza falsafa hiyo kwa kumkabidhi jukumu la kuongoza Mbio za Mwenge wa Uhuru 2025, ambapo miradi ya maendeleo itakaguliwa na kuzinduliwa pale itakapobainika kutekelezwa kwa viwango stahiki.

Share To:

Post A Comment: