MKUU wa wilaya ya Rombo mkoani Kilimanjaro, Raymond Mangwala amewataka vijana kuacha tabia ya kujipendekeza kwa viongozi kwa kupeleka maneno ya uongo na fitina na badala yake watambulike kwa kazi zao. 

Mangwala alitoa kauli hiyo jana katika kongamano la vijana wa Chama cha Mapinduzi Vyuo na Vyuo vikuu (Seneti) mkoa wa Kilimanjaro lililofanyika katika ukumbi wa CCM mkoa. 

Alisema kuwa, vijana wanapaswa kuwa wanyenyekevu na kuacha tabia ya kujitutumua kwa kuwachomea wanzao na kuwapigisha shoti kwa maneno ya uongo ili kupata nafasi au fedha kwani haitakuwa na maana yoyote katika maisha yao.

"Vijana mnawajibu wa kumuheshimu kila mtu kwani hamuwezi kujua atakuja kukusaidia katika safari ya maisha yako atakapofanikiwa mwenzako ipo siku atakuja kuwa msaada kwako mnawajibu wa kushikamana na kushirikiana na sio kupigana shoti kwa maneno ya uongo" Alisema Mangwala. 

Kwa upande wake, Katibu wa Chama cha Mapinduzi mkoa wa Kilimanjaro, Mercy Mollel alisema kuwa Chama hicho kimekuwa na utaratibu wa kuwaandaa viongozi wa badae kuanzia sasa na kuwataka vijana wa Seneti kutambua kuwa wanaandaliwa kuja kuwa viongozi wa badae. 

Naye Mwenyekiti wa Seneti Vyuo na Vyuo vikuu mkoa wa Kilimanjaro, Godfrey Deho alisema kuwa, wao kama vijana wa vyuo vikuu wameazimia hawatakuwa tayari kutumika kuvuruga amani ya Taifa na badala yake watailinda kwa nguvu zote.

"Vipo vyama vya siasa kupitia kwa viongozi wao vinaendesha harakati zinazohashiria kuvunja na kudongosha amani ya Taifa letu sisi kama vijana tunawaonya viongozi hao kuacha mara moja tabia hiyo na tutasimama nao kuhakikisha tunailinda amani yetu" Alisema Deho. 






Share To:

Post A Comment: