Makamu Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi CCM- Tanzania Bara Ndugu Stephen Wasira ameeleza kuwa kuzinduliwa kwa Benki ya Ushirika nchini baada ya takribani Miaka 40 kupita kulikofanywa na Rais Samia Suluhu Hassan leo Aprili 28, 2025 ni utekelezaji wa sera ya Msingi ya CCM iliyorithiwa kutoka kwa Vyama vya ukombozi vya Tanu na Afro- Shirazy Party vilivyokuja kuunda CCM baadae.

Wakati wa salamu za Chama Cha Mapinduzi CCM kwenye uzinduzi wa Benki hiyo Jijini Dodoma kwenye Ukumbi wa Jakaya Kikwete, Wasira ameeleza kuwa shabaha ya maendeleo ni kumkomboa mwanadamu kupitia kazi anayoifanya na kwamba Benki hiyo ya ushirika itawezesha zaidi vyama vya ushirika na Mtanzania kuweza kupiga hatua za kimaendeleo kupitia sekta ya Kilimo.

"Tumekuja hapa kwasababu kazi hii inatimiza azimio la Chama Cha Mapinduzi kuwafanya watanzania waweze kupata nafuu na waweze kupiga hatua za maendeleo yao siku hata siku. Kazi kubwa ya Chama chetu na ajenda yake ambayo haina kikomo ni kuboresha maisha ya watu ili ya leo yawe borw kuliko ya jana na ya kesho yawe bora kuliko ya leo." Amesema Makamu Mwenyekiti huyo wa CCM.

Kuzinduliwa kwa Benki hiyo kulingana na Uongozi wake ni matokeo ya kimkakati na utekelezaji wa Ilani ya CCM ya mwaka 2020/2025 kulikofanywa na Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan lengo likiwa ni kukuza tija katika sekta ya uzalishaji kwenye kufikia malengo na maono mbalimbali kuelekea mpango wa mwaka 2050 unaotaka kuifanya Tanzania kuwa miongoni mwa wazalishaji wakubwa wa chakula duniani.

Share To:

Post A Comment: