Rais wa Ukraine, Volodymyr Zelensky, ametangaza kuwa wanajeshi wa Ukraine wamewakamata raia wawili wa China waliokuwa wakipigana upande wa Jeshi la Urusi katika mkoa wa Donetsk, hatua ambayo imeibua maswali kuhusu nafasi ya China katika mozo huo unaoendelea.


Zelensky amesema kuwa hii ni dalili kuwa "idadi ya Wachina katika Jeshi la Urusi ni kubwa zaidi kuliko inavyodhaniwa." Kauli hiyo imekuja wakati ambapo China imekuwa ikijitambulisha kama mpatanishi wa amani kwenye mzozo huo, huku ikiendelea kuimarisha uhusiano wake wa karibu wa kiuchumi na kisiasa na Urusi.


Waziri wa Masuala ya Kigeni wa Ukraine, Andrii Sybiha, amesema amesikitishwa na taarifa hizo na kuhoji msimamo wa China kuhusu amani, akiongeza kuwa ubalozi wa China nchini Ukraine umeombwa kutoa maelezo rasmi kuhusu sababu za raia wake kuonekana mstari wa mbele kwenye mapigano dhidi ya Ukraine.


Hii ni mara ya kwanza kwa Ukraine kutoa taarifa rasmi inayohusisha raia wa China katika uwanja wa vita kama wapiganaji upande wa Urusi. Hadi sasa, Urusi na China bado hawajatoa majibu rasmi kuhusu tuhuma hizo.


Aidha, Kyiv na baadhi ya maafisa wa Magharibi pia wanadai kuwa Korea Kaskazini imetuma maelfu ya wanajeshi kusaidia juhudi za kijeshi za Urusi, hali inayoibua hofu ya kuongezeka kwa ushawishi

wa mataifa rafiki wa Moscow katika mzozo huo.


Kwa muda mrefu, China imekana kuipatia Urusi msaada wa kijeshi, huku ikisisitiza msimamo wake wa kutotegemea upande wowote.


Lakini tukio hill linazua maswali kuhusu uhalisia wa msimamo huo.


Wakati hayo yakijiri, mashambulizi ya ndege zisizo na rubani za Urusi yameripotiwa usiku wa kuamkia siku ya Alhamisi katika miji ya Dnipro na Kharkiv chini Ukraine, yakiwajeruhi watu 14 na kusababisha visa kadhaa vya moto.


Kwa sasa, Urusi inadhibiti karibu asilimia 20 ya ardhi ya Ukraine, huku mapigano yakiendelea kushika kasi, hasa katika maeneo ya mashariki.

Share To:

OKULY BLOG

Post A Comment: