Na. Saidina Msangi, WF, Dodoma.
Serikali imesema Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) imekuwa ikitoa elimu ya kodi kwa njia mbalimbali kwa makundi yote ya walipakodi pamoja na Vikundi vya Wanawake Wajasiriamali.
Hayo yameelezwa bungeni jijini Dodoma na Naibu Waziri wa Fedha, Mhe. Hamad Hassan Chande, alipokuwa akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalum, Mhe. Janeth Elias Mahawanga, aliyetaka kujua mpango wa Serikali wa kuanzisha madarasa ya Elimu kwa Mlipa Kodi kupitia Vikundi vya Wanawake Wajasiriamali.
‘‘TRA imekuwa ikielimisha wanawake wajasiriamali kupitia vikundi vyao mbalimbali ikiwemo chemba ya wafanyabiashara wanawake “Tanzania Women Chamber of Commerce (TWCC)” na makundi mengine ya wajasiriamali wanawake,’’alisema Mhe. Chande.
Mhe. Chande alifafanua kuwa Katika kuhakikisha utoaji elimu ya mlipa kodi unakuwa endelevu na inawafikia wajasiriamali wanawake, TRA itaendelea kushirikiana kikamilifu na Wizara husika kuimarisha mawasiliano na mtandao wa wanawake wajasiriamali ili kupitia taasisi au jumuiya zao waweze kukidhi mahitaji ya elimu ya kodi na shughuli zao za kiuchumi.
Aidha, Mhe. Chande aliongeza kuwa kupitia utoaji Elimu kwa Mlipakodi TRA imefanikiwa kuongeza idadi ya usajili wa wajasiriamali wanawake wanaojisaji kwa hiari.
Post A Comment: