Kasulu, Kigoma

Wakala ya Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) kupitia mradi wa RISE program ya uondoaji vikwazo katika barabara imefanikiwa kuwaunganisha wananchi wa kata za Kigembe, Rungwe mpya na Rusesa katika Halmashauri ya Wilaya ya Kasulu mkoani Kigoma 

Akiongea katika mahojiano maalum, Mhandisi wa TARURA wilaya ya Kasulu ambaye pia ni msimamizi wa mradi, Gervas Kadoke amesema kuwa barabara ya Kasangezi-Kigembe yenye urefu wa Km 10.46 kwa kiwango changarawe ilikuwa na changamoto ya mwamba ambapo wananchi walikuwa wakipata shida kusafiri kuzifikia huduma za kijamii na kusafirisha mazao yao kwa wakati.

Ameeleza kuwa eneo hilo lilipendekezwa kutengenezwa kupitia programu ya uondoji vikwazo katika barabara ili kuwawezesha wananchi kufanya shughuli za kiuchumi na kijamii kwa kipindi chote cha mwaka.

“Mradi umetekelezwa kwa 50% na mkandarasi anaendelea na ujenzi wa makalavati na mitaro ili kuondoa adha ya maji yanayopita kwenye makazi ya watu kuelekeza sehemu za mito, hivyo, tunaishukuru serikali kutupatia fedha ili kuboresha miundombinu ya barabara wilayani Kasulu”, amesema.

Naye, Bw. Joseph Misambo Njayi, Afisa Mtendaji wa Kijiji cha Kasangezi amesema kuwa kabla ya matengenezo ya barabara hiyo wananchi walikuwa wanasafiri kwa shida, ajali zilikuwa nyingi kutokana na njia kuwa mbovu, lakini sasa hivi ajali zimepungua watoto wanaenda shule na wakulima wanafika mashambani bila shida yoyote.

Naye, mkazi wa Kijiji cha Kasangezi Bw. Martin Sembese amesema kuwa hapo awali barabara ilikuwa haipitiki kutokana na makorongo lakini baada ya matengenezo usafiri kutoka Kasangezi hadi Kigembe umekuwa ni wa muda mfupi na wanazifikia huduma za kijamii kwa urahisi.

“Tunaishukuru serikali kutujengea barabara hii isiishie hapa tu, tunaomba na lami moja kwa moja kwa sababu barabara hii inaunganisha hadi wilaya ya Uvinza hivyo tutapata fursa ya kupeleka mazao na kufanya biashara zetu hadi Uvinza.

Share To:

Post A Comment: