Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imesaini rasmi Mkataba Mpya wa Usafiri wa Baharini wa Afrika wa mwaka 2010, hatua muhimu inayoashiria kuimarika kwa dhamira yake ya kushiriki kikamilifu katika maendeleo ya sekta ya bahari kikanda na kimataifa.
Hafla ya utiaji saini imefanyika, leo tarehe 11 Aprili 2025 katika Makao Makuu ya Umoja wa Afrika jijini Addis Ababa, Ethiopia, ambapo Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usimamizi wa Mashirika ya Meli Tanzania (TASAC), Bw. Mohamed Malick Salum, alisaini kwa niaba ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Mkataba huu ulipitishwa kwa mara ya kwanza mwaka 1994 na Jumuiya ya Umoja wa Afrika (OAU), na ukafanyiwa marekebisho mwaka 2010 na Umoja wa Afrika ili kuakisi changamoto na matarajio mapya katika sekta ya usafiri wa baharini. Lengo kuu la Mkataba huu ni kukuza mfumo wa usafiri wa baharini barani Afrika ambao ni shirikishi, salama, unaotegemewa, unaozingatia mazingira na unaochochea maendeleo ya kiuchumi.
Kwa kusaini Mkataba huu, Tanzania inathibitisha upya kujitolea kwake kwa ushirikiano wa kimataifa katika sekta ya bahari, sambamba na malengo ya Shirika la Kimataifa la Usafiri wa Baharini (IMO) ya kuimarisha usimamizi wa bahari duniani, usalama wa vyombo vya majini na ulinzi wa mazingira ya baharini.
Katika hotuba yake baada ya utiaji saini, Mkurugenzi Mkuu wa TASAC, Bw. Mohamed Malick Salum, alisema:
![]() |
“Hili ni tukio la kujivunia kwa Tanzania. Kwa kusaini Mkataba Mpya wa Usafiri wa Baharini wa Afrika, hatuchangii tu ajenda ya bara la Afrika bali pia tunafungua milango ya ushiriki mpana katika majukwaa ya kimkakati yanayokuza maslahi yetu ya kitaifa na kikanda. Ni tamko kuwa Tanzania iko tayari kushirikiana, kubuni na kuongoza katika sekta ya bahari barani Afrika.”
Moja ya manufaa makubwa ya kusaini Mkataba huu ni kwamba TASAC sasa inapata fursa ya kuwa mwanachama rasmi wa Chama cha Mamlaka za Usafiri wa Baharini Afrika (AAMA), taasisi iliyoanzishwa chini ya Mkataba huu kwa ajili ya kuratibu, kuoanisha na kukuza sera na utekelezaji wa usafiri wa baharini barani Afrika.
Post A Comment: