Waziri wa Viwanda na Biashara Mhe.Dkt.Selemani Jafo, akizungumza na Waandishi wa habari (hawapo Pichani) leo Aprili 8,2025 jijini Dodoma kuhusu ushiriki wa Tanzania katika Maonesho ya Biashara ya Kidunia Expo 2025 yatakayofanyika jijini Osaka nchini Japan.

Waziri wa Viwanda na Biashara Mhe.Dkt.Selemani Jafo, akizungumza na Waandishi wa habari  leo Aprili 8,2025 jijini Dodoma kuhusu ushiriki wa Tanzania katika Maonesho ya Biashara ya Kidunia Expo 2025 yatakayofanyika jijini Osaka nchini Japan.

Na.Alex Sonna_DODOMA

Waziri wa Viwanda na Biashara Dkt.Selemani Jafo,amesema Tanzania inatarajia  kushiriki katika Maonesho ya Biashara ya Kidunia Expo 2025 yatakayofanyika Osaka nchini Japan.

 Dkt.Jafo ameyasema hayo leo Aprili 8,2025 jijini Dodoma wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu ushiriki wa Tanzania katika maonesho hayo yanayotarajiwa kuanza rasmi 12 Aprili, 2025 hadi 13 Oktoba 2025 katika Kisiwa cha Yumeshima kilichopo Osaka nchini humo.

Kauli Mbiu ya Expo 2025 Osaka: "Kuwezesha Jamii kwa Maisha Endelevu" ambapo Tanzania imekuja na kaulimbiu ndogo isemayo 'Kuunganisha maisha' ambayo inalenga kuunganisha uzalishaji wa ndani na masoko ya nje, kuchochea uwekezaji, kuimarisha miundombinu, na kukuza biashara ya utalii.

"Tanzania ina malengo madhubuti ya kutangaza fursa za biashara, kuvutia uwekezaji, na kuonyesha urithi wake wa utamaduni na desturi katika jukwaa hili kubwa la kimataifa ambapo katika maonesho haya, Tanzania itapata nafasi ya kutangaza fursa zilizopo katika sekta mbalimbali, ikiwa ni pamoja na Afya, Nishati, Madini, Utalii, Kilimo, Uchumi wa Buluu, Sanaa na Utamaduni, na Biashara."amesema Dkt.Jafo

Aidha amesema kuwa maonesho hayo pia yatakuwa na jukwaa la kutangaza miradi ya kimkakati ya miundombinu, kama vile barabara, reli, viwanja vya ndege, bandari, nishati ya umeme na gesi, pamoja na kukuza uchumi wa buluu.

Hata hivyo amesema kuwa matokeo yanayotarajiwa katika maonesho hayo ni pamoja na uimarisha uwezo wa kuchambua taarifa za biashara na kufahamu fursa za masoko na biashara,kuongeza ajira kupitia miradi ya kimkakati inayotarajiwa kuanzishwa na kuongeza ushirikiano wa kimataifa ,kufungua milango ya uwekezaji na kuongeza idadi ya watalii na kuzindua mikataba ya kibiashara.

Pia Dkt.Jafo,amesema kuwa ushiriki wa Tanzania katika Expo 2025 Osaka unaratibiwa na Wizara ya Viwanda na Biashara, Wizara ya Biashara na Maendeleo ya Viwanda, Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, na Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, kupitia TanTrade.

Dkt. Jafo amesema kuwa siku ya Tanzania itafanyika 25 Mei 2025 na itakuwa ni moja ya matukio muhimu katika maonesho hayo ambapo Mgeni rasmi atakuwa Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Kasim Majaliwa Majaliwa.

Amesema Siku hiyo itatoa nafasi ya kutangaza fursa za biashara, uwekezaji, na utalii, huku pia ikionyesha urithi wa utamaduni wa Kitanzania.

Pia amesema kuwa kongamano la Biashara, Uwekezaji na Utalii litafanyika 26 Mei 2025, ambapo wadau wa biashara kutoka Japan na Tanzania watapata fursa ya kuungana na kubadilishana uzoefu, kuangalia uwezekano wa kuwekeza nchini, na kufanya mikataba ya kibiashara.

Amesema kuwa Serikali ya Tanzania inaendelea kushirikiana na sekta binafsi ili kutangaza na kufanikisha masoko ya bidhaa na huduma zinazozalishwa nchini lengo likiwa ni kuvutia wawekezaji na kukuza biashara za kimataifa kupitia maonesho haya.

Aidha Dkt.Jafo ametoa  wito kwa taasisi za umma, mashirika ya kimataifa, na sekta binafsi kuunga mkono ushiriki wa Tanzania katika Expo 2025 Osaka huku akisema Washiriki wanatakiwa kujisajili kupitia kiunganishi kilichotolewa kwenye matangazo rasmi au kwa kutumia QR code inayotangazwa kupitia vyombo mbalimbali vikiwemo vya habari.

Share To:

Post A Comment: