Waziri wa Madini Mhe. Anthony Mavunde ameeleza kuwa wananchi wa Kata ya Ifumbo Wilayani Chunya watapewa leseni 2 kati ya 14 za uchimbaji madini zinazomilikiwa na Kampuni ya G & I  katika bonde la Mto Zira na kutambulika rasmi kama wachimbaji halali ili wafanye shughuli za uchimbaji bila usumbufu ikiwa ni hatua ya utatuzi wa mgogoro baina  ya wananchi hao na mwekezaji.

Alisema hayo jana Aprili 28, 2025 wakati akizungumza katika Mkutano wa hadhara na wananchi wa Kata na Kijiji cha Ifumbo Wilayani Chunya ambapo aliambatana na Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira Mhe.  Khamis Hamza Chilo.

“Tunamshukuru Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa maelekezo yake kushughulikia haya mambo kwa uharaka sana na tuko hapa kwa utekelezaji wa maelekezo yake.

Baada ya kusitisha shughuli za uchimbaji madini katika bonde hilo mwishoni mwa mwezi Desemba 2024 niliunda Kamati ya Wataalam ya kutathmini athari za mazingira yaliyotokana na shughuli za uchimbaji madini katika mto Zira.

Kwa kuwa wananchi wa hapa shughuli zenu zinategemea Mto Zira, nimemwelekeza mwekezaji ili aendelee kudumisha ujirani mwema, tumekubaliana katika leseni 14 anazomiliki, atoe leseni 2 kwa ajili ya wananchi wa Ifumbo na Lupa Market ikiwa ni leseni moja kwa kila kijiji, ambako atafanya tathmini ya mazingira kabla hajakabidhi kwa serikali ya kijiji, tathmini hii ni kwa leseni 7 zilizopo Ifumbo kwa kuwa 7 zilizopo Lupa Market zimeshafanyiwa tathmini.

Kampuni ya G & I ihakikishe kuwa mazingira yanarejershwa kama yalivyokuwa awali kabla uchimbaji huu haujaanza (restoration); iweke mipaka ya leseni zao zinapoishia; Uchimbaji wa eneo la ifumbo uendelee kusimama mpaka utaratibu wa kimazingira utakapokamilika.

Kwa leseni zilizopo Kijiji cha Lupa Market, mwekezaji anaweza kuendelea na uchimbaji kwa kuwa Baraza la Taifa la Usimamizi wa Mazingira (NEMC) lilishafanya tathmini ya mazingira lakini za Ifumbo zinaendelea kusimama mpaka ukaguzi wa mazingira utakapokamilika baada ya siku 21.

Kwa upande wake, Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira Mhe. Khamis Hamza Chilo alielekeza kazi ya upandaji miti katika eneo hilo lifanywe haraka sambamba na kuzingatia utaratibu wa kufanya shughuli za kibinadamu umbali wa mita 60 kutoka kwenye ukingo wa mto kwa mujibu wa sheria.

“Nitoe maelekezo kwa NEMC itoe vibali vya ndani ya siku 21 baada ya wahusika kuomba vibali na kukamilsha utaratibu ili kuhakikisha wananchi wanafanya shughuli zao kwa tija na bila kubughudhiwa lakini pia Mameja wa NEMC wa Kanda zote kufuatilia tathmini ya mazingira yote ambako shughuli za uchimbaji madini zinafanyika  hapa nchini” alisema Chilo.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti, Mkuu wa Wilaya Chunya, Mbaraka Batenga, Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Chunya Noel Chiwanga na Mbunge wa Jimbo la Lupa Mhe. Masache Kasaka walieleza kuwa wananchi wa Chunya wamenufaika sana na shughuli za madini katika kipindi cha uongozi wako katika sekta na kuwa wananchi wa Ifumbo wakushukuru sana kwa kulipa jambo hili uzito na kulifanya kwa uharaka na hatimaye leo wamepata mrejesho.

Desemba 30, 2024 Waziri Mavunde alitangaza kusitisha shughuli za uchimbaji madini katika bonde la mto Zira na kuahidi kuunda Kamati Maalum itakayofanya tathmini ya uharibifu wa mazingira uliotokana na shughuli za uchimbaji madini na baada ya kamati hiyo kukamilisha kazi yake ataleta mrejesho.

Share To:

Post A Comment: