Serikali kupitia Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (TAWA) imewaruhusu wananchi wa Kitongoji cha Shamba la Saba kilichopo ndani ya Kijiji cha Ijia, Wilaya ya Kilombero ,Mkoani Morogoro kuvuna mazao yao yaliyolimwa ndani ya Pori la Akiba Kilombero ambalo awali lilikuwa Pori Tengefu Kilombero. 


Akizungumza na waandishi wa vyombo vya habari leo Aprili 16,2015, Kamanda wa Pori la Akiba Kilombero Bigilamungu Kagoma amesema kuwa Serikali kupitia TAWA ilitoa utaratibu wa kuorodhesha watu wote waliolima ndani ya hifadhi na kuwaruhusu wavune mazao yao pindi yatakapokomaa.


Aidha, ameongeza kuwa Shamba la Saba ni miongoni kwa Vitongoji kumi na nne (14) ambavyo Kamati ya Mawaziri Nane (8) wa Kisekta ilielekeza vitoke ndani ya hifadhi kwa ajili ya kuhifadhi vyanzo vya maji ambavyo vinachangia takribani  asilimia 65 ya maji yanayoingia katika Mradi wa Kitaifa wa Kufua umeme wa Bwawa la Nyerere.


Sambamba na hilo,  Bigilamungu amesema kuwa TAWA imetoa elimu na matangazo ya kuhamisisha wananchi kuhama kwa hiari ndani ya hifadhi kwa wananchi wa kitongoji hivyo pamoja na kuweka alama za kudumu za mipaka (vigingi) kuzunguka Pori la Akiba Kilombero.


Kwa upande wake, Afisa Mhifadhi Mkuu, anayeshughulika masuala ya Mahusiano kwa Umma - TAWA, Vicky Kamata amesema kuwa Serikali imetoa fursa hii kwa wananchi ambao tayari walishalima ndani ya hifadhi ambao walishaorodheshwa awali na sio kwa mashamba mapya na atakaebainika kuanzisha mashamba mapya atachukuliwa hatua za kisheria.


Kadhalika,Vicky ametoa rai kwa wananchi kuendelea kuheshimu sheria na kanuni zilizowekwa ikiwemo kuacha shughuli za kibinadamu katika maeneo ya hifadhi.

Ikumbukwe kuwa, Pori la Akiba Kilombero lilipandishwa hadhi kutoka kuwa Pori Tengefu Kilombero kwa tangazo la Serikali Na. 64 tarehe 17 Februari, 2023.








Share To:

Post A Comment: