Na. Saidina Msangi, WF, Dar es Salaam.
Naibu Waziri wa Fedha, Mhe. Hamad Hassan Chande (Mb), ameishukuru Serikali ya China kupitia Shirika lake la Bima SINOSURE, kwa kudhamini mkopo wa kibiashara kwa ajili ya ujenzi wa kipande cha tano (lot 5) cha Reli ya Kisasa (SGR) kutoka Isaka hadi Mwanza chenye thamani ya dola za Marekani milioni 559, kupitia mkataba uliosainiwa Oktoba 21, 2024.
Shukrani hizo alizitoa wakati wa kikao cha majadiliano kati ya Ujumbe wa Tanzania ulioongozwa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji Mhe. Prof. Kitila Alexander Mkumbo (Mb) na Ujumbe wa China ulioongozwa na Naibu Waziri wa Biashara wa Jamhuri ya Watu wa China, Mhe. Tang Wenhong, yaliyofanyika katika Hoteli ya Johari Rotana, jijini Dar es Salaam.
Pamoja na shukrani hizo, Mhe. Chande aliiomba China kuangalia uwezekano wa Kampuni ya Bima ya SINOSURE kushiriki katika ujenzi wa Kipande cha Sita cha Reli ya Kisasa kutoka Tabora hadi Kigoma chenye makadirio ya gharama ya dola bilioni 2.3.
“Fedha za kukamilisha mradi wa ujenzi wa Reli kutoka Tabaora hadi Kigoma zinatarajiwa kutoka katika vyanzo mbalimbali ambapo, dola bilioni 1.1 zinatarajiwa kutoka kwa Taasisi za Fedha za Maendeleo (DFIs), ambapo SINOSURE ni miongoni mwa wadhamini”, alisema Mhe. Chande.
Aidha, Mhe. Chande alisema kuwa ushirikiano wa Tanzania na China umewezesha Serikali ya China kufanikisha upatikanaji wa dola za Marekani milioni 108.6 kwa ajili ya Mradi wa Kuongeza Wigo wa Mawasiliano Vijijini Awamu ya Kwanza na Dola milioni 270.3 kwa ajili ya Mradi wa Usafirishaji Umeme wa 400 kV kutoka Dar es Salaam hadi Arusha, awamu ya kwanza.
Mhe Chande aliongeza kuwa uchumi wa nchi unaendelea kuimarika kutokana na uwekezaji katika miundombinu, utulivu wa uchumi jumla, mfumuko mdogo wa bei na mazingira bora ya uwekezaji.
Kwa Upande wake Naibu Waziri wa Biashara wa Jamhuri ya Watu wa China, Mhe. Tang Wenhong, alisema kuwa Serikali ya China itaendelea kuimarisha mahusiano ya kiuchumi na kidiplomasia kati ya nchi hizo mbili kwa manufaa ya wananchi wa pande hizo mbili
Post A Comment: