Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dkt. Doto Mashaka Biteko, amesema kuwa serikali itagharamia uwekaji wa miundombinu ya nishati safi ya kupikia katika Shule ya Sekondari ya Longido Samia Girls, iliyopo wilayani Longido, mkoani Arusha kqa gharama ya shilingi milioni 17, ikiwa ni sehemu ya jitihada za serikali kuhakikisha shule hiyo mpya inatumia nishati safi na salama kwa mazingira.
Dkt. Biteko ametoa ahadi hiyo wakati wa ziara yake ya kukagua maendeleo ya miradi ya maendeleo mkoani humo kuelekea maadhimisho ya miaka 61 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar.
Katika ziara hiyo, Dkt. Biteko ameagiza uongozi wa Mkoa wa Arusha, ukiongozwa na Mkuu wa Mkoa Mhe. Paul Christian Makonda, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Longido, Nassoro Shemzigwa, na Mkuu wa Wilaya, Salum Kalli, kuhakikisha vifaa vya maabara vinakamilishwa na kuwekwa kwenye maabara zote nne za sayansi huku akisisitiza kuwa wanafunzi wanapaswa kujifunza kwa vitendo badala ya kutegemea masomo ya nadharia pekee.
Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mhe. Paul Makonda, ameishukuru Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa uwekezaji mkubwa katika sekta ya elimu mkoani humo na kuahidi kuhakikisha maelekezo yote ya Naibu Waziri Mkuu yanatekelezwa kwa wakati, ikiwemo ujenzi wa uzio wa shule na upatikanaji wa vifaa vya maabara huku Akiwasihi wazazi kupeleka watoto wao shule ili waweze kutumia fursa ya elimu na kufikia ndoto zao.
Mkuu wa shule hiyo, Esther Kobelo, amesema shule hiyo ni mojawapo ya shule 26 mpya zilizoanzishwa chini ya uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan, ikiwa ni juhudi za serikali kuendeleza elimu nchini, ambapo shule hiyo ilifunguliwa Januari 7, 2024, ikiwa na wanafunzi 310 wa kidato cha kwanza na cha tano, wote wakisomea masomo ya sayansi. Shule ina walimu 16, ambapo walimu wa kike ni wanne tu, pamoja na mtaalamu mmoja wa maabara.
Post A Comment: