Wadau na Waandishi wa Habari wakifuatilia uwasilishaji wa mada na majadiliano katika siku ya kwanza ya Kongamano la Maadhimisho ya Siku ya Uhuru wa Vyombo vya Habari lililofanyika leo tarehe 28 Aprili, 2025 jijini Arusha.



Na Mwandishi Wetu.

Serikali imesema itahakikisha inafanyia kazi mapendekezo yote yatakayotolewa kwenye maazimio ya pamoja ya Waandishi wa Habari baada ya kuhitimisha Kongamano la Maadhimisho ya Siku ya Uhuru wa Vyombo vya Habari kwa mwaka 2025.

Hakikisho hilo la Serikali limetolewa leo tarehe 28 Aprili, 2025 na Katibu Mkuu Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo na Msemaji Mkuu wa Serikali Bw. Gerson wakati akitoa neno la kufunga Siku ya Kwanza ya Kongamano hilo linalofanyika jijini Arusha kwa uratibu wa Jamii Africa, UNESCO na Wizara yenyewe.

"Nimesikia maazimio ya awali mliyoyatoa hapa, ni muhimu sana na mimi nitaomba mkishakamilisha ile nakala ya mwisho mtupatie ili na sisi serikalini yale ambayo tunatakiwa tuchukue hatua tuyafanyie kazi, basi tutafanyia kazi mara moja", amesema Msigwa.
Amewapongeza wadau wote walioshiriki Kongamano hilo na kwa majadiliano waliyoyafanya ikiwemo suala la matumizi ya Akili Mnemba kwa kuwa ni jambo muhimu kwenye kazi za uandishi wa habari kwa sasa.

Bw. Msigwa amesema Serikali itaendelea kuheshimu uhuru wa vyombo vya habari nchini na kwamba hilo linajidhihirisha kwani kumekuwa na mazingira rafiki kwa Waandishi wa Habari pale wanapotekeleza majukumu yao.

"Sisi Waandishi wa Habari kwenye Awamu hii ya sita tumekuwa tukifanya kazi katika mazingira rafiki sana, kwa sababu ya maelekezo ambayo Mheshimiwa Rais (Samia Suluhu Hassan) anayasimamia," amesisitiza Msigwa na kuongeza;




"Aliyoyasema tangu siku ya kwanza alipoingia madarakani ndiyo anayoyatekeleza na sisi lazima tutekeleze maelekezo yake kuhakikisha kuna uhuru wa vyombo vya habari, kuhakikisha waandishi wa Habari hawabughudhiwi lakini kuendelea kujenga mazingira bora kwa waandishi wa habari kufanya kazi zao."

Kongamano hilo la Maadhimisho ya Siku ya Siku ya Uhuru wa Habari linatarajiwa kufungwa kesho tarehe 29 Aprili, 2025 na Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa.
Share To:

Post A Comment: