Rais Samia apongezwa kwa mageuzi makubwa ya sekta ya madini
Wizara yafikia lengo kabla ya mwaka 2025
Sekta Yatajwa Chanzo Kikuu kuingiza Fedha za Kigeni
Waziri Mavunde Awashukuru Watendaji, Watumishi na Wadau wa Sekta ya Madini
Wizara ya Madini imetangaza kuwa Sekta ya Madini nchini Tanzania imepiga hatua kubwa ya kihistoria kwa kufikia mchango wa asilimia 10.1 katika Pato la Taifa mwaka 2024, ikiwa ni mwaka mmoja kabla ya lengo lililowekwa kwenye Sera ya Madini ya mwaka 2009 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano (2021/2022 – 2025/2026).
Hayo yamebainishwa na Waziri wa Madini Mhe. Anthony Mavunde leo Aprili 23, 2025 wakati akizungumza na waandishi wa habari jijini Dodoma, na kueleza kuwa mafanikio hayo makubwa yametokana na usimamizi na maelekezo ya Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na kwa uongozi wake mahiri uliopelekea sekta hiyo kufikia hatua hiyo muhimu mapema zaidi ya matarajio.
“Ni jambo la kujivunia kuona kuwa juhudi za Serikali na wadau wa sekta hii zimezaa matunda. Mwaka 2023 tulikuwa na mchango wa asilimia 9.1 kwenye Pato la Taifa. Leo hii, tunazungumza kuhusu ongezeko hadi asilimia 10.1 kwa mwaka 2024. Hili si jambo dogo,” amesema Waziri Mavunde.
Waziri Mavunde amesema kuwa, Mafanikio hayo yametokana na mabadiliko makubwa ya kimfumo na kisheria yaliyofanyika katika Sekta ya Madini tangu kuingia madarakani kwa Serikali ya Awamu ya Sita.
Miongoni mwa hatua alizotaja kuchangia mafanikio hayo ni pamoja na: Kuongezeka kwa makusanyo ya maduhuli ya Serikali kupitia sekta hiyo, Kuanzishwa kwa minada ya madini ya vito, Udhibiti wa utoroshwaji wa madini, Kuanzishwa kwa masoko na vituo vya ununuzi wa madini nchini, pamoja na Kuanza kwa ununuzi wa dhahabu kupitia Benki Kuu ya Tanzania (BoT).
Aidha, Waziri Mavunde ametumia fursa hiyo pia kuwashukuru wadau wote wa sekta ya madini wakiwemo wachimbaji wakubwa, wa kati na wadogo pamoja na wahusika wote waliopo kwenye mnyororo mzima wa sekta ya Madini , watendaji wote wa sekta na taasisi zake kwa ushirikiano mzuri na ufanisi katika kutekeleza majukumu yao.
Vilevile, Mavunde ametoa wito kwa wawekezaji wote kuendelea kuzingatia sheria na taratibu zilizowekwa chini ya Sheria ya Madini, Sura ya 123, huku Wizara ikiendelea kutoa ushirikiano kwa wote wenye nia ya kuwekeza kwa tija.
Kwa mujibu wa Waziri Mavunde, mafanikio hayo yameonesha wazi kuwa Sekta ya Madini si tu kichocheo cha ukuaji wa uchumi bali pia ni chanzo kikuu cha fedha za kigeni, ajira, na maendeleo ya kijamii kwa Watanzania.
“Vision 2030: Madini ni Maisha na Utajiri"
Post A Comment: