MFUKO wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma (PSSSF),  unashiriki Maonesho ya Wiki ya Afya na Usalama Mahali pa Kazi (OSH- Occupational Safety and Health) yanayofanyika Kitaifa kwenye viwanja vya Maonesho Mandewa Mkoani Singida, kuanzia Aprili 24 hadi 30, 2025.

Akizungumzia ushiriki huo, Afisa Uhisano Mwandamizi wa PSSSF, Bi. Rehema Mkamba amesema, Maonesho hayo ni fursa nzuri kwa Mfuko kukutana na Wanachama na Wananchi sio tu kuwahudumia lakini pia kuwapatia elimu ya matumizi ya teknolojia katika kujihudumia wao wenyewe mahali popote na wakati wowote, maarufu kama PSSSF Kidijitali.

Aidha, kwasasa PSSSF  inaendesha zoezi la kuchukua alama za vidole kwa wanachama wake wote, kwa lengo la kuboresha huduma za PSSSF Kidijitali, amesema.

Amesema, PSSSF inaamini, utoaji huduma kwa njia ya Kidijitali unakwenda sambamba na kauli mbiu ya mwaka huu ya “Nafasi ya Akili Mnemba na Teknolojia za Kidijitali katika Kuimarisha Usalama na Afya Mahali pa Kazi.”

Kupitia PSSSF Kidijitali, Mwanachama anaweza kutumia Simu janja, Kishikwambi au computer kupata taarifa mbalimbali zinazohusiana na uanachama wake kama vile, Taarifa za Michango, Taarifa za Mafao, Taarifa za Uwekezaji, Kuwasilisha Madai mbalimbali kupitia mtandao lakini pia wastaafu wanaweza Kujihakiki kupitia simu janja. 

“Tunawakaribisha sana wanachama wetu na wanachi kutembelea banda letu ili waelimishwe namna ya kujiunga na huduma hiyo, lakini pia kupata huduma.” Alisisitiza.

Share To:

Post A Comment: