Mkoa wa Njombe umezindua rasmi kampeni ya uhamasishaji wa utoaji wa dozi ya pili ya chanjo ya Polio kwa njia ya sindano kwa watoto walio chini ya umri wa miaka mitano. Uzinduzi huo umefanyika leo tarehe 16 Aprili, 2025 katika ukumbi wa mikutano wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Njombe.
Mkuu wa Mkoa wa Njombe, Mhe. Anthony Mtaka, ambaye aliwakilishwa na Mkuu wa Wilaya ya Njombe, Mhe. Juma Sweda, aliongoza hafla hiyo na kusisitiza umuhimu wa jamii kujitokeza kwa wingi kuwapeleka watoto wao kupata chanjo hiyo muhimu ili kuimarisha kinga dhidi ya ugonjwa wa Polio.
Katika hotuba yake, Mhe. Sweda alieleza kuwa lengo la nyongeza hii ya chanjo ni kuhakikisha kuwa watoto wote chini ya miaka mitano wanapata kinga kamili dhidi ya virusi vya Polio, vinavyoweza kusababisha ulemavu wa kudumu. Alibainisha kuwa chanjo hiyo ya sindano itatolewa kwa watoto wenye umri wa wiki 14 kwa dozi ya kwanza na dozi ya pili wakifikisha miezi 9.
Aidha, aliwashukuru wataalamu wa afya kwa kazi kubwa wanayoifanya na kuwataka waendelee kutoa elimu kwa jamii kuhusu umuhimu wa chanjo, kuhakikisha ubora na usalama wake, pamoja na kuwahamasisha wazazi kuwapeleka watoto katika vituo rasmi vya kutolea huduma hiyo.
Uzinduzi huo ulihudhuriwa na wadau mbalimbali wakiwemo wataalamu wa afya, wawakilishi wa taasisi za kijamii, viongozi wa dini, pamoja na wananchi walioalikwa kushiriki kwenye tukio hilo muhimu kwa ustawi wa afya ya mtoto katika Mkoa wa Njombe.
Post A Comment: