Na WAF, TANGA

Msajili wa Baraza la Optometria Bw. Sebastiano Millanzi, amewataka wataalam wa Kada ya Optometria kuhuisha leseni zao za kutolea huduma ili waweze kutambulika katika mfumo wa wataalam wa Wizara ya Afya unaojulikana kama Health Practitioner Registration System (HPRS). 

Bw. Millanzi ameyasema hayo Aprili 10, 2025 jijini Tanga wakati wa zoezi la Usimamizi Shirikishi linalofanyika mkoani humo kwa lengo la kuona na kushauri namna bora ya utoaji wa huduma za Optometria kwa jamii. 

"Ukiwa na tabia ya kukwepa kuhuisha leseni yako kwa wakati itachochea kukwamisha kutekeleza majukumu yako kwa uhuru kwani ni kinyume cha Sheria sura ya 23 ya 2007," amesema Bw. Millanzi. 

Wakati huo huo Bw. Millanzi amewataka wamiliki wa vituo vinavyotoa huduma za optometria ambao hawajasajili vituo vyao, wasajili mara moja HPRS.

Kuhusu wamiliki ambao vituo vyao vimesajiliwa na hawajahuisha taarifa zao katika mfumo wa usajili wa vituo vinavyotoa huduma za afya, wahuishe taarifa zao mara moja ili kuepuka usumbufu wa kufungiwa lakini pia kutozwa faini isiyopungua Shilingi  Milioni Tano (5) 

Akiwa katika Hospitali ya Rufaa ya Bombo mkoani Tanga Bw. Millanzi amewaasa watumishi wa kada ya optometria katika Hopitali hiyo kuwa wabunifu ili kukisaidia kituo kuimarisha huduma zake kwa kutoa huduma bora.

"Imarisheni huduma za Mkoba za macho ili jamii hasa ya pembezoni iweze kufikiwa na huduma hizo kwani wananchi wengi wanahitaji huduma za macho lakini wanashindwa kuzipata kutokana na umbali uliopo.

Zoezi la usimamizi shirikishi limefanyika katika mkoa wa Tanga ambapo jumla ya vituo saba vilifikiwa ikiwa ni muendelezo wa ukaguzi huo inaofanyika katika mikoa mbalimbali nchini.

Share To:

Post A Comment: