Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati Mhe. Dkt. Doto Biteko amewataka Watanzania kutegemea kupata umeme wa uhakika baada ya Mradi wa kufua umeme kutoka Bwawa la Julius Nyerere uliokuwa ukisubiriwa kwa shauku kubwa na Watanzania  kukamilika  rasmi.

Waziri Biteko ameyasema hayo leo April 5, 2025 baada ya kutembelea Mradi huo akiwa ameambatana na Mawaziri ambao ni Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Mipango na uwekezaji Profesa Kitila Mkumbo na Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira Mha. Hamadi Masauni.

Amesema hivi sasa mitambo yote tisa inafanya kazi ambapo amefafanua kuwa  kukamilika kwa Mradi huo kumechangiwa na maono ya Rais wa Awamu ya Sita Mhe. Dokta Samia Suluhu Hassan ambaye aliupokea Mradi ukiwa katika asilimia 33 ya utekelezaji wake na ndani ya kipindi cha miaka minne ya Uongozi wake ameweza kuukamilisha Mradi. 

‘’Tumekuja leo tukiwa na furaha kubwa kwamba mitambo yote tisa imekamilika inazalisha umeme na nina furahi kuwajulisha Watanzania kuwa ile ndoto ya kuwa na umeme kutoka kwenye chanzo hiki kikubwa barani Afrika imekamilika, kazi iliyobaki ni kuimarisha miundombinu ya kuwafikishia watanzania umeme’’ Alisisitiza Dkt Biteko.

Dkt. Biteko amesema kutokana na nchi kuwa na uwezo wa kuzalisha umeme kwa kiwango kikubwa sasa Serikali iko katika mchakato wa kukamilisha mazungumzo na nchi ya Zambia kwa ajili ya kuwauzia umeme na tayari njia ya umeme ya kuunganisha nchi hizo mbili inajengwa.

‘’Kile ambacho tumekua tukikiongea miaka mingi kwamba Tanzania itakuwa na uwezo wa kuuza umeme nje ya nchi sasa imetimia katika kipindi hiki cha Serikali ya awamu ya sita baada ya msukumo mkubwa wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan tuna mshukuru sana Mheshimiwa Rais’’

Kwa upande wake, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Mipango na Uwekezaji Mhe.Profesa Kitila Mkumbo amesema kukamilika kwa Mradi huu ni ukombozi wa kiuchumi huku Waziri wa nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira Mhe. Hamadi Masaun amesema Tanzania imeingia katika historia barani Afrika ambapo amesema kazi kubwa iliyobaki ni kutunza vyanzo vya maji ili kuulinda Mradi.

Katika hatua nyingine Mhe Dkt Doto Biiteko amelishukuru Shirika la umeme Tanzania TANESCO kwa utekelezaji wa Mradi kwa kiwango cha kimataifa na kumpongeza Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika hilo Mha. Gissima Nyamo-Hanga kwa usimamizi na jitihada zake katika kusimamia miradi mbalimbali ya umeme.

Mradi wa Kufua Umeme wa Julius Nyerere umegharimu zaidi ya Shilingi Trilioni 6.5 ambapo mpaka sasa serikali imeshalipa zaidi ya asilimia 99.5.

Share To:

Post A Comment: