Waziri wa Madini, Mhe. Anthony Mavunde, ametoa muda wa siku 30 kwa Kampuni PMM Tanzania Limited inayoendesha na kumiliki Mgodi wa Kati wa Dhahabu wa Magambazi, uliopo katika Wilaya ya Handeni, Mkoani Tanga, kuwasilisha taarifa za kifedha na kiufundi ili kuthibitisha uwezo wake wa kuendesha mgodi huo kwa viwango vinavyohitajika kisheria.

Waziri Mavunde ametoa agizo hilo leo Aprili 6, 2025, wakati akizungumza katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika Kijiji cha Nyasa, Kata ya Kang’ata, Wilaya ya Handeni, ambapo alizungumza na wananchi wanaozunguka mradi huo.

Amesema kuwa baada ya kusikiliza pande zote za Kampuni ya PMM ma CANACO zinazohusika katika mgodi huo, ameona ni muhimu kuchukua hatua ili kuhakikisha rasilimali hiyo inaleta manufaa kwa wananchi wa Nyasa, Handeni na taifa kwa ujumla.

“Nimeagiza kuwa ndani ya siku 30, kampuni inayoliki huu mgodi, inatakiwa kuwasilisha taarifa za kifedha na kiufundi zinazoonesha uwezo wa kuendesha mgodi wa leseni ya kati, ikiwa ni pamoja na kuwa na mtaji usiopungua Shilingi Bilioni 30 kwa mujibu taarifa ya upembuzi yakinifu ya mradi na zoezi hili litaanza Aprili 8 hadi Mei 7, 2025.” Amesema Mavunde.

Sambamba na taarifa hiyo, Mhe. Mavunde amewaelekeza wamiliki hao kuhakikisha katika kipindi hicho cha siku 30, kama Kampuni haitakuwa na uwezo wa kuendesha mgodi iwe imempata mwekezaji mwenye uwezo wa kiufundi na kifedha kuendesha mgodi huo kwa tija na kwamba kinyume na hivyo, Serikali itachukua hatua za kutangaza mgodi huo kwa wawekezaji wengine wenye sifa.

Aidha, amemuelekeza Mkuu wa Wilaya ya Handeni kuandaa utaratibu maalum wa kuhesabu fedha za asilimia mbili kutoka mauzo ya awali ya dhahabu, na kuhakikisha zinawekwa kwenye akaunti ya maalum kwa ajili ya wachimbaji wadogo waliopisha maeneo hayo ya uchimbaji kama walivyokubaliana awali.

Amesisitiza kuwa Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, ina dhamira ya dhati kuhakikisha wananchi wananufaika moja kwa moja na rasilimali za madini zinazopatikana katika maeneo yao.












Share To:

Post A Comment: