OR-TAMISEMI


Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Mhe. Mohamed Mchengerwa, amewaelekeza Wakurugenzi wa Mamlaka za Serikali za Mitaa nchini kuhakikisha kuwa hawaondoi Waganga Wafawidhi wa vituo vya afya ngazi ya msingi kwa maamuzi ya hiari au kwa utashi binafsi. Badala yake wazingatie taratibu rasmi za kiutumishi na kinidhamu kwa mujibu wa miongozo iliyowekwa.

Mhe. Mchengerwa ametoa agizo hilo alipokuwa akihitimisha mkutano wa mwaka wa Waganga Wafawidhi wa vituo vya kutolea huduma za afya ngazi ya msingi, uliofanyika jijini Dodoma kwa muda wa siku mbili ambao umewakutanisha  wataalamu wa afya kutoka ngazi mbalimbali kwa ajili ya kujadili fursa, changamoto na masuala ya kitaaluma yenye lengo la kuboresha utoaji wa huduma katika ngazi ya msingi.

Katika hotuba yake, Waziri Mchengerwa amesisitiza:

“Ninawataka Wakurugenzi watumie vigezo vya kupima utendaji au ubora wa kazi za Waganga Wafawidhi wa vituo vya kutolea huduma za afya msingi—yaani Key Performance Indicators (KPI)—na si maamuzi ya mtu mmoja mmoja, nadhani nimeeleweka vizuri,”amesema.

Agizo hilo la Waziri limekuja kufuatia malalamiko kutoka kwa baadhi ya Waganga Wafawidhi waliodai kuwa wamekuwa wakiondolewa kwenye nafasi zao kwa hila, kinyume na sheria, kanuni na miongozo ya utumishi wa umma.

Share To:

Post A Comment: