Naibu Waziri katika Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia masuala ya Sera, Bunge, na Uratibu, Mheshimiwa Ummy Nderiananga amesema ni muhimu kuwa na mbinu shirikishi ili kuhakikisha watu wenye ulemavu wanajumuishwa kikamilifu katika juhudi za maendeleo kitaifa na kimataifa.
Mhe. Ummy amesema hayo aliposhiriki katika mjadala wa: Kuelekea Hatua Jumuishi za Kukabiliana na Mabadiliko ya Tabianchi Kutoka Berlin hadi Belèm na Zaidi : wakati wa Mkutano wa Kimataifa wa Watu Wenye Ulemavu uliofanyika Berlin Ujerumani tarehe 2-3 Aprili, 2025.
Amesema kuwa ingawa serikali, wadau, na mashirika ya kimataifa wanafanya kazi ya kujenga jamii jumuishi, bado watu wenye ulemavu wanakabiliwa na changamoto nyingi.
“Changamoto hizi zinahitaji suluhisho la pamoja na la muda mrefu ili kuhakikisha fursa sawa na upatikanaji wa rasilimali kwa wote, bila kumwacha mtu yeyote nyuma,” alisisitiza Mhe. Ummy.
.jpeg)
Alitaja juhudi muhimu zilizofanywa na serikali kuwa ni pamoja na: Mifumo ya Usimamizi wa Maafa, ili kuhakikisha uwakilishi wa watu wenye ulemavu na kuzingatia mahitaji yao katika kukabiliana na majanga na urejeshaji wa hali baada ya maafa; Sera za Mabadiliko ya Tabianchi, zinazolenga kuimarisha ustahimilivu wa watu wenye ulemavu kwa hatua za kukabiliana na athari za tabianchi; Mikakati Jumuishi ya Kukabiliana na Maafa, ikizingatia njia salama za uokoaji na mipango ya kuwahamisha watu wenye ulemavu; na Misaada ya Kijamii na Kisaikolojia, ili kusaidia watu wenye ulemavu wakati wa majanga.
Aliziambia nchi nyingine kuwa zinaweza kujifunza kutoka Tanzania kwa kushirikiana na mashirika ya watu wenye ulemavu, kuunda sera jumuishi, kuhakikisha miundombinu inafikika, kufanya tathmini za athari, na kutenga fedha maalum kwa ajili ya kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.
“Hatua hizi zinahakikisha kuwa watu wenye ulemavu hawataachwa nyuma katika maandalizi ya kukabiliana na majanga na ustahimilivu wa tabianchi,” alisema, huku akialika mataifa mengine kuja Tanzania kujifunza juhudi zinazofanywa na serikali.
Kuhusu hatua mahsusi za ujumuishaji wa watu wenye ulemavu katika COP30 na sera za tabianchi, Mhe. Nderiananga alisema kuwa Tanzania imeweka mfumo madhubuti wa ujumuishaji watu wenye ulemavu katika mabadiliko ya tabianchi na usimamizi wa maafa kupitia sera, sheria, na miongozo mbalimbali.
Alisisitiza kuwa Tanzania itaendelea kushirikiana na COP na wadau wengine ili kuhakikisha ujumuishaji kamili wa watu wenye ulemavu katika hatua za kukabiliana na tabianchi na itaendelea kushirikiana na mataifa mengine na mashirika ya kimataifa kuhimiza ajenda ya ujumuishaji wa watu wenye ulemavu katika COP30.
Post A Comment: