Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Ushirika nchini Tanzania iliyozinduliwa leo Aprili 28, 2025 na Rais Samia Suluhu Hassan, ameeleza kuzinduliwa kwa benki hiyo ni utekelezaji wa dhamira na maono makubwa ya Rais Samia, yaliyofanikisha wakulima wa Tanzania kupata benki yenye kuondoa changamoto ya mifumo ya fedha kutoelewana na soko la tabia za kilimo nchini kwa zaidi ya miaka arobaini sasa.

Mbele ya Rais Samia Suluhu Hassan kwenye Ukumbi wa Jakaya Kikwete Jijini Dodoma, Mura ameeleza kuwa  benki hiyo pia ni matokeo ya kimkakati ya maono ya serikali na utekelezaji wa Ilani ya CCM ya kutaka benki ya kisekta itakayojibu changamoto ya upatikanaji wa mikopo kwa wepesi na kwa njia rahisi na kwa masharti nafuu katika kuleta tija kwenye sekta ya ushirika.

Aidha katika maelezo yake, Mura ameeleza kuwa Benki hiyo inaanza na matawi manne ya Moshi  Tabora, Mtwara na Dodoma pamoja na Mawakala 58 maeneo mbalimbali huku pia bodi ya wakurugenzi ikidhamiria kuwa na Matawi matatu kufikia Mwezi Disemba katika mikoa ya Dar Es salaam, Kagera na Mkoani Mwanza.

Akizungumzia wigo wa huduma na bidhaa za benki hiyo ya ushirika, Mkurugenzi Mtendaji wa Benki hiyo mbali ya kusifu jitihada mbalimbali za Rais Samia katika kuinua na kukuza sekta mbalimbali za kiuchumi nchini, amesema Benki hiyo pia imekuja na akaunti ya Kilimo tija, ambayo itakuwa haina gharama yoyote katika uendeshaji wake ili kuwapa fursa wakulima kuweza kuweka akiba isiyokatwa chochote na Benki hiyo.

Mura ameeleza kuwa Benki hiyo si tu Taasisi ya kifedha bali pia ni vuguvugu la kubadilisha maisha ya watanzania akieleza kuwa kufikia mwaka 2030, benki hiyo imedhamiria kuwa asilimia 50 ya Watanzania wawe wanatumia huduma za kibenki kwa kuhakikisha kuwa walau wanachama wote Milioni kumi wa vyama vya ushirika wawe wamejiunga na Benki hiyo kufikia 2030.

Share To:

Post A Comment: