Serikali itaendelea kuimarisha Mipango na Bajeti kwa ajili ya ununuzi wa vifaa vya maabara na kemikali za maabara ili kuhakikisha vinapatikana kwa uhakika na wakati kwa ajili ya ujifunzaji na kufundishia.
Haya yamebainishwa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais-TAMISEMI, Mhe Mohamed Mchengerwa wakati wa kujibu hoja za wabunge kuhusu mpango wa Serikali wa kupeleka vifaa vya maabara kwenye shule 26 za sayansi za wasichana za mikoa, bila kuathiri mipango iliypowekwa ya upelekaji wa vifaa vya maabara katika shule nyingine za sekondari nchini.
Amesema vifaa vya maabara kwa shule 486 vimenunuliwa katika awamu mbili (2) na usambazaji wa awamu ya kwanza unahusisha shule 231, zikiwemo shule 26 za sayansi za wasichana na hadi sasa shule 8 kati 26 za wasichana zimepokea vifaa hivyo na usambazaji katika shule 18 zilizobakia unaendelea.
Amesema vifaa vya maabara na kemikali kwa awamu ya pili kwa ajili ya shule 255 zilizobaki vinaendelea kupokelewa na kusambazwa na pia Serikali imenunua na kusambaza kemikali za maabara katika shule za sekondari 231 ngazi ya kata.
Kuhusu kubuni chanzo cha kudumu cha fedha kwa ajili ya ununuzi wa vifaa vya maabara kwa shule za sekondari nchini, Mchengerwa amesema Serikali imekuwa ikitoa fedha za ununuzi wa vifaa vya maabara kwa shule za sekondari nchini kupitia Ruzuku ya Uendeshaji wa Shule.
Pia ununuzi wa vifaa vya maabara hufanyika kupitia utekelezaji wa miradi mbalimbali ikiwemo Mradi wa Kuimarisha Elimu ya Sekondari (SEQUIP), Mpango wa Lipa kulingana na Matokeo (EP4R) na michango ya wadau.
Hivyo, Mchengerwa amesema Serikali itaendelea kuimarisha Mipango na Bajeti kwa ajili ya ununuzi wa vifaa vya maabara na kemikali za maabara ili kuhakikisha vinapatikana kwa uhakika na wakati kwa ajili ya ujifunzaji na kufundishia.
Kuhusu hoja ya usimamizi na uendeshaji wa shule za mchepuo wa kiingereza katika halmashauri, Mchengerwa amesema Ofisi ya Rais - TAMISEMI imeipokea hoja hii na itafanya uchambuzi kwa kushirikiana na Wizara inayosimamia Sera ya Elimu ili kupata utekelezaji mzuri wahojahusika.
Post A Comment: