Na Benny Mwaipaja, Dar es Salaam
Waziri wa Fedha, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb), amelihakikishia Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF) kwamba, Serikali itaendelea kufanya maboresho ya sera na mipango yake kwa kuhakikisha sekta mbalimbali za kiuchumi na kijamii pamoja na kuimarisha sekta binafsi zinapewa kipaumbele.
Dkt. Nchemba amesema hayo wakati akifunga vikao vya majadiliano kati ya Serikali na Timu ya Wataalam kutoka Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF), baada ya kukamilisha tathimini ya awamu ya tano ya utekelezaji wa program ya Extended Credit Facility-(ECF), inayohusisha mkopo nafuu kwa ajili ya kuimarisha uchumi wa nchi kupitia sekta za uzalishaji na huduma za jamii pamoja na awamu ya pili ya utekelezaji wa program ya kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi kupitia dirisha la Resilient and Sustainable Fund (RSF) kutoka Shirika hilo.
Akifunga vikao hivyo katika Kikao cha majumuisho kilichofanyika Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Jijini Dar es Salaam, Dkt. Nchemba, alieleza kufurahishwa kwake na taarifa iliyowasilishwa na Kiongozi wa Timu hiyo Bw. Nicolas Blancher, inayoonesha kuwa Tanzania imetekeleza ipasavyo vigezo vilivyowekwa na Shirika hilo katika mipango hiyo ya ECF na RSF.
Aliahidi kuwa Serikali itaendelea kusimamia ipasavyo utekelezaji wa programu hizo mbili zenye thamani ya dola za Kimarekani bilioni 1.832, ambapo kiasi cha dola bilioni 1.1 ni kwa ajili ya Mpango wa kuimarisha Uchumi wa nchi kupitia sekta za uzalishaji na kiasi cha dola milioni 786 ni kwa ajili ya Mpango wa nchi kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi, ambapo program hizo mbili zinatekelezwa katika kipindi cha miaka minne kuanzia mwaka 2022/2023 hadi 2025/2026.
Kwa upande wake, Kiongozi wa Timu ya Wataalam kutoka IMF waliofanya tathimini hiyo, Bw. Nicolas Blancher, alisema kuwa tathimini yao ya awamu ya tano imeonesha kuwa Tanzania imetekeleza vizuri mpango wa ECF na RSF na kushauri hatua kadhaa zinazotakiwa kuendelea kuchukuliwa ikiwemo kuimarisha zaidi huduma za jamii na kuendelea kuimarisha mazingira bora ya kufanyabiashara na uwekezaji.
“Matarajio ya uchumi wa Tanzania ni mazuri kwakuwa utaendelea kukua kwa kasi, huku mfumuko wa bei ukiendelea kuwa chini, nakisi ya mauzo na manunuzi ya bidhaa na huduma nje ya nchi ikipungua, na upatikanaji wa fedha za kigeni ukiongezeka” alisema Bw. Blancher.
Aliongeza kuwa hatua za kuwianisha vizuri mapato na matumizi ya serikali katika mwaka wa fedha wa 2025/26, zitasaidia kuhifadhi uhimilivu wa deni la serikali, huku zikilinda matumizi yenye kipaumbele katika huduma za kijamii.
Bw. Blancher alisema kuwa kuendelea kutekeleza sera za kukabiliana na athari na changamoto za mabadiliko ya tabianchi, zinazoungwa mkono na mpango wa RSF, kutasaidia kujenga ustahimilivu katika kushughulikia madhara ya mabadiliko ya tabianchi.
Alisema kuwa mapendekezo ya tathimini hiyo yatapelekwa mbele ya Bodi ya Wakurugenzi wa Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF) na kwamba uamuzi utakaotolewa na Bodi utaiwezesha Tanzania kupokea ufadhili wa dola za Marekani milioni 441.
Tanzania imefanyiwa Tathimini ya Awamu ya Tano ili iweze kupata fedha kutoka IMF kwa ajili ya kutekeleza miradi mbalimbali ya kiuchumi na kijamii ambapo hadi sasa Program ya ECF imepokea kiasi cha dola za Marekani milioni 754.3 kati ya dola za Marekani bilioni 1.1 na kiasi kingine cha dola za Marekani milioni 55 zimepokelewa kupitia dirisha la RSF, mradi wenye thamani ya dola za Marekani milioni 786.
Kikao hichi kilihudhuriwa na Katibu Mkuu Wizara ya Fedha, Dkt. Natu El-Maamry Mwamba, Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania, Bw. Emmanuel Tutuba, na Manaibu Gavana, pamoja na Maafisa Waandamizi wa Serikali na wajumbe wa Timu ya Tathimini kutoka Shirika la Fedha la Kimataifa-IMF.
Post A Comment: