Katika hatua ya kihistoria ya kuwezesha mapinduzi ya kiuchumi kupitia teknolojia na ubunifu wa vijana, Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kushirikiana na wadau wa maendeleo imezindua rasmi mpango wa uwezeshaji kwa wabunifu wa Kitanzania wenye thamani ya shilingi bilioni 4.6.

Mpango huo unatekelezwa kupitia ushirikiano kati ya Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH) na CRDB Foundation, ukiwa na lengo la kugeuza mawazo ya wabunifu kuwa miradi hai ya biashara na viwanda.

Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Adolf Mkenda, akizindua mpango huo, alisema kuwa kati ya hizo bilioni 4.6, Serikali kupitia COSTECH imetoa dhamana ya shilingi bilioni 2.3, huku CRDB Foundation ikitoa kiasi kilichosalia kama mikopo nafuu kwa wabunifu waliokidhi vigezo.

“Hili ni jambo la kipekee. Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan ameelekeza wazi kuwa vijana wabunifu wawezeshwe, na leo tumeona matokeo ya dhamira hiyo. Serikali haikubaki nyuma, imetoa dhamana ya bilioni 2.3 ili kuhakikisha hakuna mkwamo wa kifedha kwa wabunifu wetu,” alisema Prof. Mkenda.

Ameongeza kuwa Tanzania haiwezi kufikia maendeleo ya kweli bila kutoa kipaumbele kwa ubunifu, hasa kwa vijana, ambao ndio nguvu kazi ya taifa.

Alisisitiza kuwa serikali iko tayari kushirikiana na taasisi za umma na binafsi katika kuhakikisha kuwa kila wazo lenye tija linapata msukumo wa kifedha, kitaalamu na kiutendaji.

Katika hafla hiyo, Prof. Mkenda aliwapongeza CRDB Foundation kwa ujasiri wao wa kuwekeza kwa wabunifu wa Kitanzania, akisema huo ni mfano wa taasisi binafsi zinavyoweza kuchangia maendeleo ya kitaifa. “Taasisi nyingine zijifunze kutoka CRDB Foundation.

Vijana wetu hawahitaji huruma, wanahitaji fursa. Na tukiwapa fursa, watafanya maajabu,” alisema huku akiwasihi wadau wengine kujitokeza kuwekeza kwa wabunifu wa ndani.

Mkurugenzi Mkuu wa COSTECH, Dkt. Amos Nungu, alieleza kuwa zaidi ya wabunifu 400 kutoka mikoa mbalimbali nchini tayari wamenufaika na programu za uwezeshaji za COSTECH, na wengi wao wapo katika hatua ya kupokea mikopo.

Alibainisha kuwa mikakati kama hii ni utekelezaji wa moja kwa moja wa ahadi za Rais Samia Suluhu Hassan katika kuwawezesha vijana na kutumia maarifa, sayansi, teknolojia, na ubunifu kama suluhisho la changamoto za maendeleo.

Miongoni mwa maeneo yanayopatiwa kipaumbele ni pamoja na teknolojia za kidijitali, akili-bandia (AI), na suluhisho bunifu kwa changamoto za kijamii kama afya, kilimo, na elimu.

Profesa Mkenda alisisitiza umuhimu wa kuingiza masomo ya akili-undi kwenye mitaala ya elimu ili kuandaa kizazi chenye uwezo wa kukabiliana na ushindani wa soko la kimataifa.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa CRDB Foundation, Bi. Tully Esther Mwambapa, alisema kuwa taasisi hiyo imeamua kushirikiana na COSTECH kama njia ya kuendeleza miradi yenye mwelekeo wa biashara na athari kwa jamii.

“Tunatambua kuwa ubunifu ni injini ya maendeleo. Kupitia uwekezaji huu, tunawaleta vijana karibu na fedha, maarifa, na mitandao ya ukuaji. Lengo letu ni kusaidia kubadilisha maisha yao na jamii kwa ujumla,” alisema Bi. Mwambapa.

Kwa ujumla, uzinduzi huu unafungua ukurasa mpya wa maendeleo ya ubunifu nchini. Historia imeandikwa—wakati umefika kwa wabunifu wa Kitanzania kuinuka, kushirikiana na wadau, na kuwa sehemu muhimu ya ujenzi wa uchumi wa viwanda na maarifa.

Kupitia uwekezaji huu wa bilioni 4.6, Tanzania sasa inatengeneza mazingira wezeshi kwa vijana kuandika kesho yao kupitia maarifa, teknolojia na uthubutu.
Share To:

TANGA RAHA BLOG

Post A Comment: