Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko amewaasa Watanzania kuendeleza fikra za Mwl. Nyerere kwa kuwekeza katika sekta za elimu, kilimo, viwanda, teknolojia na biashara ndogo ndogo zinazotegemewa na wananchi wengi ili kukuza uchumi jumuishi.

Aidha, Serikali na sekta binafsi zinapaswa kushirikiana ili kuhakikisha uwekezaji unaleta tija kwa wananchi wa kawaida. \n\nDkt. Biteko amesema hayo leo Aprili 11, 2025 jijini Dar es salaam wakati aliposhiriki katika Kongamano la Kumbukizi ya Kuzaliwa Kwa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere katika Chuo cha Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere. 

Amesema Kongamano hilo lenye mada inayosema Maono ya Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere katika Elimu, Uwekezaji na Ujenzi wa Taifa lenye Amani kwa Maendeleo ya Watu ni fursa ya kufanya tafakuri kwa baadhi ya mambo ambayo Baba wa Taifa aliyaamini, aliyaishi na anaendelea kukumbukwa nayo.

“Maono ya Mwalimu kuhusu uwekezaji kwa maendeleo yalilenga kuimarisha uchumi wa Taifa kwa misingi ya usawa na uwajibikaji wa pamoja.

Alisisitiza kuwa uwekezaji lazima uwalenge wananchi na kuhakikisha kwamba rasilimali za Taifa zinatumika kwa manufaa ya wote. Alipinga mifumo ya kiuchumi inayozalisha matabaka na ukosefu wa haki, huku akihimiza ujamaa na kujitegemea,” amesema Dkt. Biteko.

 Ameongeza kuwa Mwl. Nyerere alitamani kuona elimu inampa mwanafunzi maarifa ya kumwezesha kuchangia maendeleo ya jamii yake na sio ya kumtenga na mazingira yake. Aidha, jamii inapaswa kujiuliza ikiwa sasa elimu inawajenga Watanzania kuwa raia wenye uwezo wa kutatua matatizo yao na kuchangia maendeleo yao na ya Taifa kwa ujumla.

Amebainisha kuwa katika dunia ya sasa yenye ushindani mkubwa wa kiteknolojia na kiuchumi, ni muhimu kuwekeza katika elimu inayozingatia maendeleo ya sayansi, teknolojia, ubunifu na stadi za maisha ili kujiletea maendeleo ya kweli.










Share To:

Post A Comment: