Katika kuhakikisha taifa linapata viongozi bora wa kesho, taasisi zisizo za kiserikali za HakiElimu na The African Leadership Initiative For Impact (ALI For Impact) zimezindua programu maalum ya kuwawezesha vijana walioko mashuleni kupata maarifa na ujuzi wa uongozi.
Mpango huu mpya unalenga kuwa chachu ya mabadiliko kwa kuwapa wanafunzi nafasi ya kutambulika, kuendelezwa na hatimaye kuchukua nafasi kama viongozi wa baadaye katika sekta mbalimbali zenye uhitaji mkubwa wa uongozi thabiti na wenye maadili.
Akizungumza na wanahabari jijini Dar es Salaam mapema leo, Makumba Munezi, Mkuu wa Idara ya Utafiti, Uvumbuzi na Uchambuzi wa Sera wa HakiElimu, alisema kuwa programu hiyo imeanzishwa baada ya kubainika mapungufu makubwa katika maandalizi ya viongozi waliopo sasa.
“Tumeona kuwa kuna upungufu mkubwa wa maandalizi ya viongozi katika sekta mbalimbali. Tumegundua kuwa mojawapo ya sababu ni kutotambuliwa kwa watoto na vijana wenye vipaji vya uongozi wakiwa bado shuleni,” alisema Makumba.
Makumba alieleza kuwa kwa muda mrefu kumekuwa na ukosefu wa miundombinu na mifumo ya wazi ya kuwaendeleza vijana wenye vipaji, hali ambayo imekuwa ikisababisha vipaji hivyo kupotea bila kufikia hatua ya juu.
Kwa mujibu wake, uwekezaji katika kundi hili la vijana ni msingi wa kuandaa kizazi kipya cha viongozi wenye dira, uzalendo na uwezo wa kuleta mabadiliko chanya katika jamii na taifa kwa ujumla.
Programu hii ni sehemu ya juhudi za mashirika haya mawili kuchangia maendeleo ya taifa kwa njia ya kuwekeza kwenye elimu ya uongozi kwa vijana wadogo. Kwa sasa, hatua za awali za utekelezaji wa mpango huu zimeanza katika baadhi ya shule, na matarajio ni kuupanua zaidi kwa kushirikiana na wadau wengine wa maendeleo.
Post A Comment: