Sakata la Mbunge wa Arusha Mjini, Mrisho Gambo, limechukua sura mpya baada ya Spika wa Bunge, Dk. Tulia Ackson, kuielekeza Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge kumhoji mbunge huyo pamoja na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Mohamed Mchengerwa.

Maagizo hayo yametolewa leo bungeni mara baada ya Waziri Mchengerwa kupewa nafasi ya kutoa ufafanuzi juu ya tuhuma nzito zilizotolewa na Gambo wakati wa mjadala wa makadirio ya bajeti ya TAMISEMI kwa mwaka wa fedha 2025/2026.

Katika mchango wake, Gambo alidai kuwa Jiji la Arusha linajenga jengo la utawala lenye ghorofa nane kwa gharama zinazodaiwa kufikia zaidi ya Shilingi bilioni tisa, akidai kuwa ni gharama kubwa isiyoeleweka na kuomba uchunguzi wa kina kufanyika juu ya matumizi hayo.

Tuhuma hizo zilimlazimu Spika kutoa maelekezo kwa Waziri Mchengerwa kufanya uchunguzi na kuwasilisha majibu bungeni, jambo ambalo Waziri huyo amelitimiza leo kwa kutoa maelezo ya kina ndani ya Bunge.

Hata hivyo, baada ya Waziri kuwasilisha taarifa yake, Gambo aliomba muongozo wa Spika na kudai kuwa Waziri Mchengerwa ametoa taarifa za uongo. Kutokana na mvutano huo, Spika Dk. Tulia ameagiza Kamati ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge kuanza mara moja mchakato wa kuwasikiliza wawili hao na kuwasilisha ripoti yao wiki ijayo bungeni.

“Mnazijua vizuri kanuni zetu na tunakaribia kuhitimisha vikao vya Bunge. Kamati itawasikiliza na kisha italeta ripoti itakayoonyesha nani aliyezungumza kweli na nani alisema uongo. Baada ya hapo, hatua stahiki zitachukuliwa kulingana na ripoti hiyo,” amesema Spika Tulia.

Tayari Kamati hiyo imeanza kazi leo tarehe 23 Aprili, 2025 na inatarajiwa kuhitimisha uchunguzi na kuwasilisha taarifa bungeni wiki ijayo.

"Mnazijua kanuni zetu vizuri na tupo mwishoni bunge hivyo hakuna mtu hasiye zijua kanuni zetu hivyo Kamati itawasikiliza harafu itakuja kusema hapa nani muongo nani mkweli na kisha hatua zitachukuwa baada ya hapo" Spika Tulia

Source : Nipashe

Share To:

Post A Comment: