Akisisitiza umuhimu wa kuwa na Shukrani kama ambavyo imehubiriwa hii leo kwenye Ibada ya Pasaka kwenye Kanisa la KKKT Sinoni Jijini Arusha, Mbunge wa Arusha Mjini Mhe. Mrisho Gambo amemtaja Rais Samia kama Kiongozi aliyeweka alama nyingi za vielelezo vya miradi ya maendeleo Arusha Mjini, akimshukuru kwa kutenga fedha nyingi za kutekeleza miradi ya Maendeleo Arusha.
Mhe. Gambo aliyeshiriki Ibada ya Pasaka kwenye Kanisa hilo na kuchangia shughuli mbalimbali za maendeleo zinazoendelea kanisani hapo, ameeleza kwamba kuwa na Mwanamke Kiongozi kuanzia ngazi ya familia ni baraka na chanzo cha Maendeleo, akisema kwa Arusha pekee Rais Samia amefanikiwa kukuza uchumi wa wananchi kwa asilimia kubwa kwa kipindi kifupi ambacho amekuwa Rais wa Tanzania.
Mhe. Mrisho Gambo amewaambia waumini wa kanisa hilo kuwa Rais Samia Suluhu Hassan kwa muda mfupi aliokuwa madarakani, ametoa Bilioni 286 kwaajili ya ujenzi wa Uwanja wa michezo Mirongoine kata ya Olmot, lakini pia amesisimua sekta ya utalii Mkoani humo kupitia filamu ya The Royal Tour, suala ambalo limekuza uchumi na kutoa ajira kwa Vijana na wajasiriamali wengi wa Mkoa wa Arusha, akieleza kuwa mambo hayo kwa Arusha yanafanikiwa kutokana na ushirikiano uliopo kati ya Ofisi yake na Wenyeviti wa Serikali za Mitaa na Madiwani wa Arusha Mjini.
Gambo pia amezungumzia mradi wa Uendelezaji Miji Tanzania (TACTICS)ambapo ameeleza kuwa kutokana na jitihada za Rais Samia, fedha zimetolewa na Tenda imeshatangazwa ambapo kutafanyika Ujenzi wa Masoko makubwa mawili ya Kilombero na Morombo, yatakayokwenda sambamba na ujenzi wa Kituo kikuu cha Mabasi Arusha itakayojengwa eneo la Bondeni City.
Akizungumzia alama zilizowekwa na Rais Samia kwa Kata ya Sinoni, Mhe. Gambo ameeleza kuwa Rais Samia atatoa Milioni 250 za awali kwaajili ya ujenzi wa Kituo cha afya Sinoni, akitoa pia fedha katika Bajeti ijayo ya serikali kwa ajili ya Ujenzi wa shule ya Sekondari Sinoni ili kupunguza masafa marefu ya wanafunzi kufuata huduma ya elimu kwenye shule za nje ya Sinoni.
Mhe. Gambo amemshukuru Rais Samia pia kwa kuirejesha Arusha kwenye uenyeji wa mikutano ya Kitaifa na Kimataifa, akieleza kuwa mikutano hiyo imekuwa sehemu ya kukuza uchumi wa wananchi wa Arusha Mjini kupitia biashara na Ujasiriamali ambao wamekuwa wakiufanya na kuleta tija kutokana na mwingiliano na ugeni mkubwa wa watu mbalimbali wanaofika Arusha kuhudhuria Mikutano na warsha za ndani na nje ya Tanzania.
Post A Comment: