Na. Joseph Mahumi, Washington
Waziri wa Fedha, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba Mb), amekutana na kufanya Mazungumzo na Mkurugenzi Mtendaji wa Masuala ya Utawala na Uendeshaji wa Benki ya Dunia, Bi. Anna Bjerde, kando ya Mikutano ya Majira ya Kipupwe ya IMF na Benki ya Dunia, inayofanyika Jijini Washington D.C, nchini Marekani, ambapo pamoja na mambo mengine, Dkt. Nchemba aliishukuru Benki hiyo kwa mchango mkubwa wa maendeleo ya Tanzania kupitia miradi mbalimbali inayopata fedha kutoka Taasisi hiyo pamoja na kuonesha nia ya kusaidia ujenzi wa Mradi wa Reli ya kisasa (SGR)
Aidha, katika kikao hicho, alitambulishwa Makamu wa Rais Mpya wa Benki ya Dunia anayesimamia Kanda ya Afrika Mashariki na Kusini, Bw. Ndiamé Diop, ambaye ameteuliwa hivi karibuni baada ya Bi. Victoria Kwakwa kumaliza muda wake.
Kikao hicho kimehudhuriwa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha, Dkt. Natu El-maamry Mwamba, Balozi wa Tanzania nchini Marekani, Mhe. Dkt. Elsie Kanza, Katibu Mtendaji wa Tume ya Mipango, Dkt. Fred Msemwa, Kamishna wa Idara ya Usimamizi wa Deni la Serikali, Wizara ya Fedha, Bw. Japhet Justine, Kamishna Msaidizi kutoka Idara ya Fedha za Nje, Wizara ya Fedha, Bw. Robert Mtengule, Mwakilishi Mkazi wa Benki ya Dunia nchini Tanzania, Bw. Nathan Belete na viongozi wengine waandamizi wa Serikali na Benki ya Dunia.





Post A Comment: