Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Mashaka Biteko (Mb), ameweka  jiwe la msingi mradi wa ujenzi wa jengo jipya la utawala la Chuo cha Maendeleo ya Jamii Tengeru (TICD) Aprili 25, 2025 katika ziara yake ya kikazi mkoani Arusha.

Mhe. Dkt. Biteko ameipongeza TICD na Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum kwa usimamizi madhubuti ya mradi wa ujenzi wa jengo hilo ambalo litamaliza changamoto ya uhaba wa ofisi kwa watumishi wa Chuo hicho.

‘’Nimekagua mradi huu naona mmeamza vizuri na mtamaliza vizuri na nawapongeza kwa usimamizi mzuri’’ amesema Mhe. Dkt. Biteko.

Mapema akiwasilisha taarifa ya utekelezaji wa mradi kwa Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mkuu wa Chuo cha Maendeleo ya Jamii, Dkt. Bakari George, ameeleza kuwa TICD inatekeleza mradi huo  utakaogharimu kiasi cha shilingi Bilioni 5.6 mpaka kukamilika kwake.

Dkt. Bakari ameeleza kuwa jengo hilo litakuwa la ghorofa tatu na jumla ya  ofisi 44 pamoja na kumbi tano za mikutano zenye uwezo wa kuchukua watu 545 kwa wakati mmoja.

Kwa mujibu wa Dkt. Bakari jengo hilo ni la kisasa lenye  mifumo yote muhimu ambayo ni mfumo wa umeme, mfumo wa kuzuia majanga ya moto, mfumo wa TEHAMA, mfumo wa kiyoyozi, mfumo wa maji safi na maji taka.

Naye Katibu Mkuu wa Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Dkt. John Jingu, ambaye aliambatana na viongozi wengine katika ziara hiyo amemhakikishia Naibu Waziri Mkuu Dkt. Biteko kuwa Wizara itaendelea kusimamia utekelezaji wa mradi huo kwa ukaribu ili uweze kukamilika kwa wakati na kutumika kwa maendeleo ya Chuo hicho.











Share To:

Post A Comment: