Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt.Doto Biteko ameliomba Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuidhinisha Bajeti ya Wizara ya Nishati kwa mwaka 2025/2026 ya kiasi cha shilingi Trilioni 2.2 ambapo asilimia 96.5 ya Bajeti yote ni kwa ajili ya Miradi ya Maendeleo na asilimia 3.5 ni kwa ajili ya Matumizi ya Kawaida.
Akiwasilisha Bajeti hiyo tarehe 28 Aprili, 2025 bungeni jijini Dodoma, Dkt.Biteko ametaja vipaumbele mbalimbali vya Wizara ya Nishati kwa mwaka 2025/2026 ikiwemo kuendelea kuimarisha uzalishaji, usafirishaji na usambazaji wa umeme, pamoja na kufikisha Gridi ya Taifa katika mikoa iliyosalia ya Rukwa, Kagera, Lindi na Mtwara.
“Mhe. Spika, kipaumbele kingine ni kuendelea na usambazaji wa nishati katika vitongoji, maeneo ya migodi, kilimo, viwanda na pampu za maji pamoja na vituo vya afya ili kuwezesha shughuli za uzalishaji na utoaji wa huduma bora kwa wananchi.” Ameeleza Dkt.Biteko
Ametaja kipaumbele kingine kuwa ni upatikanaji wa umeme wa uhakika kwa maendeleo ya kiuchumi na kijamii kwa kutekeleza Mradi wa Kuimarisha Gridi ya Taifa na kufanya matengenezo na ukarabati wa mitambo ya kuzalisha umeme.
Pia kuhamasisha na kuwezesha watanzania kutumia nishati safi ya kupikia ikiwa ni utekelezaji wa Mkakati wa Taifa wa Matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia (2024-2034) na Mpango wa Taifa wa Nishati wa Mwaka 2025 – 2030.
Dkt. Biteko ametaja kipaumbele kingine kuwa ni kuhakikisha kunakuwa na upatikanaji wa umeme wa uhakika kwa maendeleo ya kiuchumi na kijamii kwa kutekeleza Mradi wa Kuimarisha Gridi ya Taifa na kufanya matengenezo na ukarabati wa mitambo ya kuzalisha umeme.
Pia, kuendelea kuwezesha upatikanaji wa bidhaa za mafuta vijijini kupitia ujenzi wa vituo vya mafuta katika maeneo hayo.
Dkt. Biteko ameongeza kuwa kipaumbele kingine cha Bajeti ya 2025/2026 ni kutekeleza shughuli za utafutaji, uendelezaji na usambazaji wa mafuta na gesi asilia na kutekeleza miradi ya kielelezo na kimkakati ya mafuta na gesi asilia.
Vilevile kusimamia na kuhakikisha nchi inakuwa na uhakika wa upatikanaji wa bidhaa za mafuta ya petroli pamoja kuimarisha matumizi ya gesi asilia (CNG) katika vyombo vya moto.
Ameongeza kuwa kipaumbele kingine ni kuendelea kutekeleza shughuli za kiudhibiti kwa kuimarisha ushiriki wa wazawa katika Sekta ya Nishati pamoja na kuimarisha nguvu kazi na kuwezesha upatikanaji wa vitendea kazi ili kuimarisha tija na ufanisi katika utendaji kazi.
Pia kuongeza mchango wa nishati jadidifu katika uzalishaji wa umeme na ushiriki wa Sekta Binafsi katika maendeleo ya Sekta ya Nishati na kuanza utekelezaji wa Mpango wa Taifa wa Nishati wa Mwaka 2025 - 2030 (National Energy Compact 2025 - 2030) kuhusu upatikanaji na uunganishaji wa umeme kwa wananchi.
Awali Dkt.Biteko alilieleza Bunge la Tanzania kuhusu mafanikio mbalimbali ya Bajeti ya Wizara ya Nishati kwa mwaka wa fedha 2024/2025 ikiwemo kukamilika kwa mradi wa kielelezo wa kuzalisha umeme kwa Kutumia Maji wa Julius Nyerere (JNHPP) – MW 2,115 na ujenzi wa njia ya kusafirisha umeme msongo wa kilovoti 400 yenye urefu wa kilomita 160 kutoka kituo cha kuzalisha umeme cha Julius Nyerere hadi Chalinze mkoani Pwani.
Ametaja mafanikio mengine kuwa ni kukamilika kwa Ujenzi wa kituo cha kupokea na kupoza umeme cha Chalinze na kuingiza umeme unaozalishwa JNHPP kwenye Gridi ya Taifa pamoja na kukamilika kwa njia ya kusafirisha umeme msongo wa kilovoti 400 kutoka Singida hadi Arusha.
Mafanikio mengine yaliyopatikana katika Bajeti ya 2024/2025 ni kuongezeka kwa uwezo wa mitambo ya kuzalisha umeme iliyounganishwa katika Gridi ya Taifa kutoka MW 1,601.84 Mwaka 2020/21 hadi MW 4,031.71 na kukamilika kwa Ujenzi wa kituo cha kupokea na kupoza umeme cha Chalinze na kuingiza umeme unaozalishwa JNHPP kwenye Gridi ya Taifa.
Pia kukamilika kwa ujenzi wa njia ya kusafirisha umeme ya msongo wa kilovoti 400 kutoka Nyakanazi hadi Kigoma na kuunganisha Mkoa wa Kigoma kwenye Gridi ya Taifa na kufanikiwa kuokoa kiasi cha Shilingi bilioni 58.4 zilizokuwa zinatumika kwa mwaka kwa ajili ya ununuzi wa mafuta ya dizeli katika mkoa wa Kigoma.
Katika usambazaji wa umeme vijijini, Dkt. Biteko amesema kuwa katika mwaka wa fedha 2024/2025, Serikali imefikisha miradi ya umeme katika vijiji vyote 12,318 vya Tanzania Bara kutoka vijiji 506 vilivyokuwa vimeunganishiwa umeme mwaka 2007 wakati REA inaanzishwa. Pia, kufikisha umeme kwenye vitongoji 33,657 kati ya 64,359 sawa na asilimia 52.
Dkt. Biteko ametaja mafanikio mengine kuwa ni kukamilika kwa ujenzi wa njia ya kusafirisha umeme ya msongo wa kilovoti 132 yenye urefu wa kilomita 115 kutoka Tabora hadi Urambo na hivyo kuimarisha upatikanaji wa umeme Urambo pamoja na kuongezeka kwa uhamasishaji na matumizi ya nishati safi ya kupikia ikiwemo usambazaji wa mitungi ya gesi ya kupikia 266,000 na majiko banifu 5,000 kwa wananchi.
Mafanikio mengine ya Bajeti ya 2024/2025 ni kuimarika kwa upatikanaji wa umeme katika mikoa ya Lindi na Mtwara kutokana na kufungwa kwa mtambo wa kuzalisha umeme kwa kutumia gesi asilia wa MW 20 katika eneo la Hiyari – Mtwara pamoja na kuongezeka kwa wateja waliounganishiwa umeme nchini kutoka 2,766,745 Mwaka 2020/21 hadi 5,449,278 mwezi Aprili, 2025 ikiwa ni ongezeko la asilimia 97.
Katika Sekta ndogo ya Gesi Asilia, Dkt. Biteko amesema kuwa kumekuwa na ongezeko la mtandao wa usambazaji wa gesi asilia nchini kutoka kilomita 102.54 Mwaka 2020/21 hadi kilomita 241.58 mwezi Aprili 2025 ambao umewezesha kuunganishwa kwa jumla ya nyumba 1,514, taasisi 13 na viwanda 57.
Vilevile kumekuwa na ongezeko la ushiriki wa TPDC katika Kitalu cha uzalishaji wa gesi asilia cha Mnazi Bay kutoka asilimia 20 hadi asilimia 40 na kutolewa Leseni ya Uendelezaji wa Kitalu cha kuzalisha gesi asilia cha Ntorya kwa TPDC ambayo itashirikiana na Kampuni ya ARA Petroleum katika uendelezaji wa kitalu hicho.
Mafanikio mengine ni kuongezeka kwa vituo vya kujaza gesi asilia (CNG filling stations) kwenye vyombo vya moto kutoka vituo viwili (2) Mwaka 2020/21 hadi vituo tisa (9) mwezi Aprili 2025 pamoja na kuongezeka kwa ushiriki wa Watanzania katika shughuli za utafutaji na uzalishaji wa gesi asilia hadi asilimia 90 ikilinganishwa na mwaka 202.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini, Mhe. David Mathayo ameeleza kuwa katika Bajeti ya mwaka 2024/2025, Wizara ya Nishati imetekeleza vipaumbele vyake kwa kiwango cha kuridhisha ambapo Kamati hiyo imepongeza Viongozi Wakuu wa Wizara ya Nishati pamoja na Watendaji kwa ushirikiano mkubwa wanaoutoa kwa Kamati hiyo lengo likiwa ni kuhakikisha kuwa Sekta ya Nishati inakuwa na mafanikio.
Kuhusu Bajeti ya Mwaka 2025/2026 Kamati imeishauri Wizara ya Nishati masuala mbali ikiwemo kuzidi kufuatilia upatikanaji wa fedha za utekelezaji wa miradi ya nishati, malipo ya fidia kwa wananchi wanaopisha miradi,TANESCO kuongeza kasi ya ukarabati wa miundombinu ya umeme pamoja na kuendeleza miradi ikiwemo ya kusafirisha umeme ili wananchi wapate umeme wa uhakika.
Post A Comment: