SERIKALI ya wilaya ya Tanga imeipongeza Taasisi ya Bilal Muslim Mission of Tanzania kwa kujitolea kuendesha kambi maalumu ya matibabu ya macho bure wananchi wa wilaya hiyo ambapo pia wanapatiwa dawa , Miwani na kufanyiwa upasuaji wa mtoto wa jicho mara baada ya kugundulika kuwa na tatizo hilo.
Akizindua kambi hiyo iliyaonza 5 April 2025 katika shule ya Sekondari Usagara Mkuu wa wilaya ya Tanga Japhari Kubecha ameipongeza taasisi hiyo ambayo inaendesha kambi hiyo kwa mara ya pili tangu ile ya mwaka 2019 kwa kuwatibu wananchi ambapo wengi wamekuwa na changamoto ya macho baada ya kufanyiwa vipimo.
Aidha Kubecha amesema kuwa Serikali ya wilaya itaendelea kutoa ushirikiano kwa kwa taasisi hiyo pamoja na wadau wengine ili kuhakikisha kuwa wananchi wanapata huduma mbalimbali ikiwemo za afya.
"Tumeona hamasa ni kubwa , ofisi ya mbunge pamoja na Serikali wametangaza kwa muda mfupi lakini muitikio umekuwa ni mkubwa sana sisi kama Serikali ya wilaya hatuna cha kuwalipa taasisi ya Bilal Muslim Mission of Tanzania zaidi ya kuwashukuru wametufanyia hisani kubwa mno wananchi na sisi kama Serikali ya wilaya tuwahakikishie kwamba tutaendelea kushirikiana nao kwa Kila hali"amesema Kubecha.
Aidha Mkuu huyo wa wilaya amempongeza mbunge wa Jimbo la Tanga Ummy Mwalimu kwa kuwaleta Wadau hao kuja kutoa matibabu hayo kwa wananchi ambapo wananchi wameendelea kujitokeza kuitumia fursa hiyo ambayo wengi wangeshindwa kuvipata kwa wakati kutokana na gharama za matibabu.
"Sisi kama Serikali ya wilaya ya Tanga tunampongeza sana mbunge wa jimbo la Tanga kwa namna ambavyo ameendelea wote tunafahamu kwamba mbunge hana fedha za kuhudumia watu lakini jinsi anavyotafuta fursa na kuzileta katika eneo lake binafsi nimpongeze na kumshukuru kwa hiki ambacho amekifanya ni sehemu ya kuzisaidia Serikali yetu chini ya Dkt. Samia Suluhu Hassan " amesema Kubecha.
Mbunge wa Jimbo la Tanga Ummy Mwalimu amewapongeza wananchi wa Jiji la Tanga wanaoendelea kujitokeza kupatiwa huduma hiyo ambayo itahitimishwa April 7,2024 huku akiwaasa kufuata maelekezo na ushauri wa wataalamu wa afya ikiwemo kuepuka kuvaa Miwani bila kufanyiwa vipimo ili kuepukana na madhara mbalimbali ya kiafya.
Aidha Ummy ameendelea kuwashukuru taasisi ya Bilal Muslim Mission of Tanzania Kwa jinsi wanavyohudumia wananchi pamoja na kampuni ya simu ya Yas ambao ndio waliodhamini kambi hiyo huku akiwaahidi wananchi kuendelea kuwaletea huduma mara tu zinapopatikana.
"Niendelee kuwashukuru wadau wetu kutoka Bilal Muslim Mission of Tanzania Kwa kuleta kambi hii hapa Tanga pamoja na wadau wengine better charitable trust na mtandao wa Yas na Mimi niwaahidi watu wa Tanga kuwa wajibu wangu kama mbunge ni kutafuta fursa kwaajili ya wananchi wa wilaya ya Tanga" amesema Ummy.
Daktari bingwa wa macho kutoka taasisi ya Bilal Muslim Mission of Tanzania Hussein Abas ambaye pia ni mratibu wa macho kwa Mkoa wa Tanga amesema kuwa kuwa katika Mkoa wa Tanga zaidi ya asilimia 50 ya wananchi wameathirika na magonjwa ya macho ikiwemo mtoto wa jicho ambapo wengi wanalazimika kufanyiwa upasuaji ili kuondokana na changamoto hiyo.
Mpaka sasa ikiwa ni siku ya pili zaidi ya watu 1500 waliojitokeza katika kambi hiyo wametibiwa na kupatiwa dawa pamoja na Miwani huku 84 kati yao waligundulika kuwa na tatizo la mtoto wa jicho kufanyiwa upasuaji katika hospitali ya rufaa ya mkoa wa Tanga Bombo.
Kambi hiyo ambayo imeanza kufanyika April 5 ikitarajiwa kuhitimishwa April 6 wananchi wameendelea kujitokeza kwa kupatiwa matibabu ambapo wengi wameeleza kupona akiwemo Mwanarabu Yusuph aliyesumbuliwa na matatizo ya macho tangu mwaka 2005.
Post A Comment: