Na Oscar Assenga,Tanga. 

Katibu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Tanga, Shabani Hamisi, amemshukuru Mbunge wa Jimbo la Tanga Mjini, Ummy Mwalimu, kwa kuandaa mashindano ya Oddo Ummy Cup kwa kushirikiana na chama cha mpira mkoa wa Tanga (TRFA) akisema kuwa ni hatua muhimu katika kukuza vipaji vya vijana jijini humo.

Akizungumza kama mgeni rasmi kwenye fainali ya mashindano hayo, Hamisi alisema kuwa michezo ni ajira kwa vijana kama zilivyo ajira nyingine, na ni njia mojawapo ya kuimarisha mahusiano na kuwaepusha na vitendo viovu.
"Kwa niaba ya Mheshimiwa Mbunge, nipo hapa kama mgeni rasmi kuhakikisha kuwa mashindano haya yanakuwa chachu kwa vijana katika kujikwamua kiuchumi. Michezo ni ajira, na pia ni njia bora ya kujenga nidhamu na mahusiano bora katika jamii," alisema.
Aidha Alisema kuwa Ummy Mwalimu amekuwa mstari wa mbele kuhakikisha vijana wa Tanga wanashiriki katika michezo mbalimbali na kutumia fursa zinazojitokeza. Alisisitiza kuwa mbunge huyo yuko tayari kushirikiana na vijana katika nyanja tofauti ili kuwawezesha kufikia ndoto zao.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Chama cha Soka Mkoa wa Tanga (TRFA), Martin Kibua, aliwataka wachezaji na makocha kuzingatia sheria za mchezo, huku akipiga marufuku wachezaji kuhama hama katika timu bila kufuata utaratibu rasmi.
Katibu wa Mbunge wa Jimbo la Tanga Mjini, Hassan Nyelo, alieleza kuwa ligi ya mwaka huu imekuwa ya kihistoria kutokana na udhamini mkubwa uliotolewa na Mbunge huyo, ikiwa ni mara ya kwanza kwa ligi ya wilaya kupata udhamini wa asilimia 100, ikijumuisha michezo 98 na zawadi zote.
"Mheshimiwa Mbunge amekuwa akiunga mkono jitihada za Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, hasa katika sekta ya michezo. Ameahidi kuendeleza juhudi hizi kwa michezo mingine zaidi baada ya mpira wa miguu," aliongeza.
Nyelo alihitimisha kwa kuwaomba vijana na wakazi wa Tanga kuendelea kumuunga mkono Mhe. Oddo Mwalimu kwa juhudi zake za kukuza maendeleo ya vijana kupitia michezo.




Share To:

TANGA RAHA BLOG

Post A Comment: