Wabunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wamepitisha kwa kauli moja bajeti ya Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) kwa mwaka wa fedha 2025\/26 yenye takribani Shilingi trilioni 11. 783 kwa ajili ya wizara na taasisi zilizo chini yake.

Kwa mujibu wa Waziri Mchengerwa Bajeti hiyo imeongezeka kutoka Shilingi trilioni 10.125  zilizotengwa mwaka 2024\/25 hadi kufikia Shilingi trilioni 11.783 na kuwa na ongezeko la  zaidi ya Sh trilioni 1.66.

Shilingi trilioni 3.95 zimepitishwa kwa ajili ya Miradi ya Maendeleo ambapo kati ya fedha hizo Shilingi trilioni 2.5 ni fedha za ndani, ikijumuisha Shilingi bilioni 613.44 za mapato ya ndani ya halmashauri na Shilingi trilioni 1.45 ni fedha za nje.

Pia Shilingi trilioni 7.84 ni kwa ajili ya matumizi ya kawaida yanayojumuisha mishahara Shilingi trilioni 6.3 na matumizi mengineyo Shilingi trilioni 1.53 ikijumuisha Shilingi trilioni 1. 067 za mapato ya ndani ya halmashauri.

Akijibu hoja za wabunge Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Mhe Mohamed Mchengerwa amesema kuwa anatambua uwepo wa changamoto za ujenzi, ukarabati na matengenezo ya barabara katika maeneo mbalimbali nchini. Katika kushughulikia changamoto hiyo serikali imeendelea kutenga fedha kupitia TARURA kwa ajili ya ujenzi, matengenezo na ukarabati wa Barabara ambapo bajeti imeongezeka kutoka shilingi bilioni 275.00 mwaka 2020\/21 hadi shilingi bilioni 772.19 mwaka 2024\/25 sawa na ongezeko la asilimia 180.8 ya fedha za ndani.

Pia Waziri Mchengerwa amesema kuwa Ofisi ya Rais - TAMISEMI inatambua umuhimu wa kuboresha mazingira ya kufundishia na kujifunzia ambapo imeendelea kujenga na kukarabati miundombinu ya elimu pamoja na kuendeleza mazingira ya maeneo hayo.

Serikali imeendelea kuwekeza katika utoaji wa Elimumsingi na Sekondari ambapo Mpango wa Elimumsingi bila Ada umeongezewa bajeti yake kutoka shilingi bilioni 249.66 mwaka 2020\/21 hadi shilingi bilioni 510.96 mwaka 2025\/26 kwa mwaka sawa na ongezeko la shilingi bilioni 261.30 sawa na asilimia 104.66.

Share To:

Post A Comment: