WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema Serikali ya awamu ya sita imejenga shule za wasichana katika mikoa 26 zenye michepuo ya masomo ya sayansi ambazo hadi sasa ujenzi wake umegharimu sh. bilioni 121.55.

 

“Wakati anaingia madarakani Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan alieleza azma yake ya kumsaidia mwanamke. Katika kutekeleza azma hiyo, Serikali ya awamu ya sita imejenga shule za wasichana katika mikoa 26 zenye michepuo ya masomo ya sayansi. Hadi sasa, ujenzi wa shule hizo umegharimu shilingi bilioni 121.55 za Tanzania na tayari wanafunzi 10,274 wameshadahiliwa,” amesema.

 

Ametoa kauli hiyo leo mchana (Jumatano, Aprili 9, 2025) Bungeni jijini Dodoma, wakati akiwasilisha taarifa ya Mapitio ya Utekelezaji wa Kazi za Serikali kwa mwaka 2024/2025 na mwelekeo wa kazi zake na makadirio ya mapato na matumizi ya fedha za Ofisi ya Waziri Mkuu na Ofisi ya Bunge kwa mwaka 2025/2026.

 

Waziri Mkuu amesema mbali na ujenzi wa shule hizo, Serikali imeanzisha programu ya ufadhili kwa wanafunzi wa elimu ya juu (Samia Scholarship Program) kwenye fani za sayansi, teknolojia, ubunifu, uhandisi, hisabati na tiba wenye ufaulu wa kiwango cha juu. “Shilingi bilioni 6.63 zimekwishatolewa tangu kuanza kwa programu hiyo na kunufaisha wanafunzi 1,313,” amesema.

 

Waziri Mkuu Majaliwa amelieleza Bunge kwamba Serikali inatoa ufadhili wa mikopo kwa wanafunzi wa elimu ya vyuo vya kati wanaosoma stashahada za fani za ufundi. “Tangu kuanzishwa kwa mpango huo, shilingi bilioni 20.08 zimetolewa na kunufaisha wanafunzi 7,732. Pia, Serikali imeanzisha Mfuko wa  Wabunifu unaojulikana kama Samia Innovation Fund ili kusaidia wabunifu kuchochea biashara za ubunifu na kuongeza fursa za ajira,” ameongeza.

 

Akitoa mwelekeo wa Serikali kwa mwaka 2025/2026, Waziri Mkuu amesema Serikali itaendelea kuimarisha ubora wa mafunzo ya amali, kununua vifaa vya kufundishia kwa vyuo vya VETA na Vyuo vya Maendeleo ya Wananchi; kuendelea na ujenzi wa vyuo vya ufundi, kuongeza mikopo kwa wanafunzi wa elimu ya kati na elimu ya juu. “Serikali itaendelea kuboresha elimu ya awali, msingi, sekondari na ualimu kwa kuimarisha mafunzo kwa walimu, kuongeza uwiano wa vitabu kwa wanafunzi na kuimarisha elimu maalum, na kuongeza bajeti ya fedha za mikopo na ufadhili wa wanafunzi.”

 

Wakati huohuo, Waziri Mkuu amesema hali ya upatikanaji wa maji imeimarika kutokana na utekelezaji wa miradi ya ujenzi na uboreshaji wa miundombinu ya kutolea huduma ya maji vijijini na mijini. Amssema jumla ya miradi 1,633 imetekelezwa ambapo kati ya hiyo, miradi 1,335 ni ya vijijini na miradi 298 ya mijini.

 

Akielezea kuhusu kuongezeka kwa upatikanaji wa huduma ya maji mijini na vijijini, Waziri Mkuu amesema: “Miradi hiyo imeongeza kiwango cha upatikanaji wa huduma ya maji vijijini kutoka wastani wa asilimia 70.1 mwaka 2020 hadi asimilia 79.6 mwaka 2025. Kwa upande wa mijini kutoka wastani wa asilimia 84 mwaka 2020 hadi asilimia 90 mwaka 2025. Kutokana na ongezeko hilo  wananchi 12,547,526 wamenufaika na huduma ya maji safi na salama.”

 

Amesema pamoja na mafanikio makubwa yaliyopatikana katika kipindi cha Serikali ya Awamu ya Sita katika mwaka 2024/2025, Serikali imeendelea kutekeleza miradi mbalimbali ikiwemo mradi wa Same – Mwanga – Korogwe; Mugango – Kiabakari – Musoma na imekamilisha uchimbaji wa visima 925, ambapo kila jimbo la uchaguzi Tanzania Bara limepata wastani wa visima vitano vya maji.

 

Kuhusu mwaka 2025/2026, Waziri Mkuu amesema Serikali itaendelea kukamilisha miradi mikubwa ya maji, kuimarisha ushirikiano na sekta binafsi katika utekelezaji na uendeshaji wa miradi ya maji na kuimarisha ufuatiliaji wa ubora wa maji yanayotumiwa na wananchi.

 

Kwa mwaka 2024/2025, Waziri Mkuu ameliomba Bunge liidhinishe sh. 595,291,624,000/- ambapo kati ya fedha hizo, sh. 183,821,010,000/- ni kwa ajili ya matumizi ya kawaida na sh. 411,470,614,000/- ni kwa ajili ya matumizi ya maendeleo kwa Ofisi ya Waziri Mkuu na taasisi zilizo chini yake.

 

Pia Waziri Mkuu ameliomba Bunge liidhinishe sh. 186,793,635,000/- kwa ajili ya Mfuko wa Bunge. Kati ya fedha hizo, shilingi 174,960,303,000 ni kwa ajili ya matumizi ya kawaida na shilingi 11,793,332,000 ni kwa ajili ajili ya matumizi ya maendeleo.

Share To:

Post A Comment: