Bashungwa aagiza Jeshi la Polisi kushughulikia wizi wa kahawa

Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan inaendelea kusimamia sera nzuri na mifumo madhubuti ya usimamizi na uuzaji wa kahawa, kwa lengo la kuhakikisha wakulima wa zao hilo wanaendelea kunufaika kwa kupata bei nzuri na yenye tija.

Kauli hiyo imetolewa na Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi na Mbunge wa Karagwe, Innocent Bashungwa, tarehe 17 Aprili 2025, wakati akifunga kambi ya Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM) katika Wilaya ya Karagwe, mkoani Kagera.

Bashungwa alieleza kuhusu changamoto zilizokuwepo katika vyama vya ushirika, ambako baadhi ya viongozi wachache walihusika katika kuwaumiza na kuwanyonya wakulima wa kahawa wilayani humo.

"Kipindi kile haikuwa kazi rahisi. Mnajua vita iliyokuwepo kwenye masuala ya ushirika. Niliwaambia viongozi wangu wa chama kuwa niko tayari kuwa mbunge wa kipindi kimoja, lakini siwezi kuwa sehemu ya unyonyaji wa wakulima wa kahawa," alisema Bashungwa.

Aidha, Bashungwa amemuagiza Mkuu wa Polisi Wilaya ya Karagwe (OCD) kuhakikisha anashughulikia aina yoyote ya uhalifu unaowalenga wakulima wa kahawa, ikiwemo usalama wa mashamba, ili mkulima aweze kunufaika na jitihada zake.

"OCD, tunavyoingia kwenye msimu wa kahawa, kutokana na bei kuwa nzuri, kutakuwepo na ongezeko la vitendo vya uhalifu mashambani. Wewe na askari wako hakikisheni mnadhibiti hali hiyo na kumlinda mkulima hadi kahawa yake iuzwe katika vyama vya msingi," alisisitiza.

Pia, Bashungwa ameeleza kuwa Serikali imehakikisha vyama vya ushirika vinaendeshwa kwa kuzingatia taratibu sahihi ili kuleta ushindani wa bei na kuhakikisha wakulima wanapata faida stahiki.








Share To:

Post A Comment: